Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kufungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10 Desemba, 2020 jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza na washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10 Desemba, 2020 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu wakimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kabla ya kufungua kongamano hilo.
**************************************
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 11 Desemba, 2020
Serikali inazingatia haki za binadamu na kupambana na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha taasisi za umma nchini zinatoa huduma bora kwa wananchi na bila upendeleo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) alipokuwa akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10 Desemba, 2020 jijini Dodoma.
Mhe. Mkuchika amesema, suala la haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa ni mtambuka, ndio maana taasisi zote zinazojishughulisha na utawala bora zimekutana na wadau wa sekta ya umma na binafsi katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu mwaka huu ili kujadili na kutoa mapendekezo yatakayoboresha mapambano dhidi ya rushwa na uzingatiaji wa haki za binadamu.
Mhe Mkuchika ameeleza kuwa, uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za binadamu kwa mwaka huu ulifanyika kwa kuzungumza na Waandishi wa Habari ili washiriki kutoa elimu kwa umma dhidi ya rushwa na uzingatiaji wa haki za binadamu.
Taasisi zilizoshiriki kuandaa maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Uzingatiaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na Watumishi kwa Ustawi wa Utawala Bora na Haki za Binadamu nchini”.