**********************************
NA MWAMVUA MWINYI, Bagamoyo
Des 11
MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Muharami Mkenge, amehimiza halmashauri ya Bagamoyo kubuni vyanzo vipya vya mapato vitavyoisaidia kuinua pato la halmashauri hiyo.
Mkenge alitoa kauli hiyo alipozungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Madiwani, ambapo alisema vyanzo hivyo vitasaidia kuongeza wigo wa mapato vikishirikiana na vilivyopo hivi sasa.
“Niwaombe wataalamu kubuni vyanzo vipya vya mapato, ili kuiwezesha halmashauri izidi kupiga hatua za kimaendeleo,” alisema Mkenge.
Nae Diwani wa Viti Maalumu Ummy Matata alisema, wakazi wanavamia maeneo ya mji huo wakitumia kigezo cha uwekezaji ambapo wanapopatiwa ardhi kubwa hawaitumii kwa malengo husika hivyo kukwamisha maendeleo.
Apsa Kilingo alielezea kukwama kwa kuendelea kwa Halmashauri hiyo kutokana na maeneo mengi kuhodhiwa na watu wachache wanaitumia kigezo cha uwekezaji, hali inayochangia maeneo mengi kuwa mapori.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mohamed Usinga aliutaka uongozi sekta ya afya kuboresha huduma, ambapo alisema kuwa wakati wa Kampeni ya Ubunge alitembelea maeneo mengi ambapo malalamiko makubwa yaligusia afya.
“Katika ziara ya Kampeni tulipokuwa tunamtembelea mgombea Ubunge Muharami Mkenge tumepokea malalamiko mengi yanayohusiana na sekta ya afya, wananchi wanakwenda kupata husyma wanaambiwa dawa hakuna”, alisema Usinga.