Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akitoa maelekezo kwa uongozi wa Bodi ya Filamu Tanzania kutafuta wataalaum watakaoanzisha mfumo wa kidigitali nchini utakao kuwa unasambaza kazi za filamu za Tanzania kama ilivyo Nextfil, leo Desemba 11, 2020 katika kikao cha makabidhiano ya ofisi na Waziri Mstaafu wa Wizara hiyo Dkt.Harrison Mwakyembe (kulia). Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega.
Naibu Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Abdallah Ulega akisisitiza katika kipindi cha uongozi wake ataendelea kulinda amali za nchi na kuulinda Utamaduni, leo Desemba 11, 2020 katika kikao cha kukabidhiana ofisi na Waziri mstaafu wa wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) (wa kwanza kulia) Waziri wa wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa, (wa kwanza kushoto) Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akitoa taarifa ya mambo mbalimbali aliyoyafanya waziri mstaafu wa wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) kwa Waziri Mhe. Innocent Bashungwa (hayupo pichani) leo Desemba 11, Jijini Dodoma katika kikao cha makabidhiano ya ofisi kwa mawaziri hao mbele ya menejimenti na wakuu wa taasisi.
Waziri mstaafu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiwasilisha ombi kwa Waziri wa wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa la kusimamia mambo muhimu yaliyoainishwa katika Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1999 kuingizwa katika Mitaala ya somo la historia kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akiwaapisha mawaziri, kwa lengo la kukuza na kuendeleza utamaduni wa taifa na uzalendo, Makabidhiano hayo yamefanika leo Desemba 11, 2020 katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Waziri mstaafu wa wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akikabidhi taarifa ya utekezaji wa majukumu yake katika kipindi cha uongozi wake kwa Waziri wa Wizara hiyo Innocent Bashungwa (wa pili kushoto), leo Desemba 11,2020 katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma zilizopo, mbele ya Viongozi wa Menejimenti na Wakuu wa Taasisi, (kushoto) Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega (wa kwanza kushoto).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (watatu kushoto) akimkabidhi zawadi ya picha iliyochorwa Waziri mstaafu wa wizara hiyo Dkt.Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) leo Disemba 11,2020 Jijini Dar es Salaam, wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, wapili kushoto ni Naibu Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Abdallah Ulega.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (aliyeketi watatu kushoto) na waziri mstaafu wa wizara hiyo Dkt.Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa menejimenti ya wizara na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara leo Desemba 11, 2020 Jijini Dodoma mara baada ya makabidhiano ya ofisi kwa mawaziri hao, (wa kwanza kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, wa pili kushoto ni Naibu Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Abdallah Ulega na wa kwanza kushoto waliokaa ni Naibu Katibu Mkuu Dkt.Ally Possi.
PICHA NA ANITHA JONAS (WHUSM)
*****************************************
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa amesema kuwa mambo yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake Dkt.Harrison Mwakyembe katika sekta anazozisimamia atayaendeleza ili matarajio ya kuundwa kwa kwa Wizara hiyo yafikiwe.
Mhe.Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 11, 2020 wakati akipokea Ofisi kutoka kwa Waziri mstaafu Dkt.Harrison Mwakyembe ambapo ameeleza kuwa ataendelea kushauriana na naye katika masuala mbalimbali ya wizara hiyo kutokana na uzoefu aliyonao, huku akisitiza kuwa mahusiano mazuri na watu katika maeneo mbalimbali ya kazi na jamii ni muhimu kwa sababu manufaa mengi.
“Tulishirikiana na wewe katika kuhamisha Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja wizara hii,nimatumaini yangu tutaendelea kushirikiana katika sekta zote za wizara hii”, alisema Mhe. Bashungwa.
Akiendelea kuzungumza Waziri Bashungwa alisema kuwa tayari ameaviagiza Vyama vya Michezo kuwasilisha mpango mkakati wa namna ya kuendesha michezo nchini, huku akisisitiza suala la Makampuni ya Michezo ya Kubahatisha kuchangia katika ustawi wa Timu za Taifa.
Aidha,Mhe.Bashungwa ameiagiza Bodi ya Filamu Tanzania kuona namna ya kuanzisha mfumo ambao utatumika kuuza kazi za filamu kwa mfumo wa kidigitali kama ilivyo ‘Netflix’ kwani itasaidia wasanii kusambaza kazi zao kwa urahisi na pia kuchangia katika pato la taifa ambapo alisisitiza kuwa “Msanii kiwanda chake ni kichwa chake”.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa jambo la kuwa na Shule za Michezo (Sports Academy) ni jambo la msingi ambalo uongozi wao utalifanyia kazi na kuweka mkazo katika michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ili timu ya taifa itokane na vijana hao.
“Tumejipanga kuhakikisha tunalinda Utamaduni wa Taifa Letu, vijana tunaowajibu wa kuhakikisha tunu za nchi pamoja na maadili ya nchi yetu tunayalinda, na katika sekta ya Sanaa tunatambua Sanaa ni ajira hivyo tutasaidia kuikuza”,alisema Mhe.Ulega.
Awali akiwakaribisha viongozi hao Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Mwakyembe kumekuwepo na mafanikio mengi ikiwemo ongezeko la Bajeti pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika wizara hiyo.
Katika ufafanuzi wake Dkt. Abbasi alisistiza kuwa Dkt.Mwakyembe alisimamia vyema sekta ya Habari ambapo alihakikisha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, inafuatwa pamoja na Kanuni zake ambapo alisisitiza kuwa sekta ya habari ni taaluma na vyombo vya habari vina haki na wajibu.
“Katika uongozi wako Dkt.Mwakyembe ulifanya mambo mengi, ulitatua mgogogo kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kampuni ya Startimes ambao uliyokuwa umedumu kwa muda mrefu, umeongoza kuanzishwa kwa Tanzania Safari Chaneli, umefanya maboresho makubwa katika shirika hilo ikiwemo kuanzishwa kwa kipindi cha Aridhio, umesimamia sekta ya michezo kwa kutunga Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa pamoja na kuunda Kamati ya Kusimamia Haki za Wasanii”,alisema Dkt.Abbasi.
Kwa upande Waziri huyo aliyemaliza muda wake Dkt.Harrison Mwakyembe amewashauri viongozi hao kutambua umuhimu wa kuundwa kwa Wizara hiyo tangu enzi za Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambapo lengo lilikuwa ni kulinda historia ya nchi.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wizara hiyo ina Sekta ya Utamaduni ambayo ni kiini na roho ya taifa kwa kuwa inaeleza mambo mbalimbali ya taifa ikiwemo lugha ya Kiswahili, umuhimu wa Wimbo wa Taifa ambapo ni lazima kuimbwa shuleni kila siku na kwenye shughuli mbalimbali za kitaifa ambapo Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 imeeleza kuwa ni jambo hilo ni la lazima.
Vilevile Dkt.Mwakyembe amesema kuwa sekta ya habari inatambulika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, wananchi wana haki ya kupata taarifa na habari sahihi na sekta ya michezo na Sanaa zinatoa fursa kwa vijana ikiwemo kujiajiri hivyo ni muhimu zikaendelea kuendelezwa.