*******************************
NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
Des 11
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewahakikishia wananchi wa Kata ya Pera na Chalinze kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za migogoro ya Ardhi katika Halmashauri hiyo .
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Pera ,aliwahakikishia wananchi kuwa wamejipanga vizuri kumaliza kero za mipaka hasa ile isiyokwisha kati ya Kitongoji cha Pingo na Chamakweza ambao umedumu kwa takribani miongo Miwili.
Awali akiwa katika Kitongoji cha Pingo, Mbunge aliweza kufanya mkutano wa wazi na Wananchi ambapo pia aliongozana na watalaam mbalimbali wa Idara pamoja na viongozi wa ngazi ya Vitongoji, Kata na Wilaya wakiwemo Wanasiasa.
Mbunge amewaahidi Wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano huku akiwashukuru kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi CCM ikiwemo kumpatia asilimia zaidi ya 94 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Katika mkutano huo ambao Mbunge alipokea pia kero mbalimbali zinazowakabili Wananchi ikiwemo migogoro ya mipaka,
Mgogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, Fursa za TASAF, mikopo ya Jamii , Afya na mengineyo.
Hata hivyo Mbunge aliweza kutolea ufafanuzi baadhi ya kero za Wananchi ambazo zimeanza kufanyiwa kazi na kuwakumbusha kuwa serikali haikuwa imelala ilikuwa inafanya kazi, huku zingine akiahidi kuzichukua kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.