**************************
Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kimesheherekea maadhimisho ya sherehe za miaka 59 tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa kupanda miti katika viwanja vya inapojengwa ofisi ya wilaya ya chama hicho na kuendesha harambee ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la ofisi za wilaya hiyo linalojengwa katika kata ya Buswelu.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mgeni rasmi Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela Ndugu Renatus Mulunga mbali na kuwaasa vijana kuifahamu historia ya Uhuru wa Tanganyika, Akawataka kushirikiana na kuwa wamoja katika kujiletea maendeleo sambamba na kuendesha harambee ya uchangiaji wa gharama za kukamilisha ujenzi wa ofisi za wilaya ambapo mifuko ya saruji ilikusanywa na miche 187 ya miti ya matunda na kivuli ilipandwa ambayo ilitolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula
‘.. Mbunge wetu amechangia mifuko ya saruji kukamilisha ofisi ya chama chetu na sisi madiwani wake tumemuunga mkono kwa kila mmoja kutoa mfuko minne kukamilisha ofisi hii, Ili shughuli za kila siku za chama chetu ziendelee kutekelezwa ..’ Alisema
Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula, Ndugu Kazungu Safari Idebe akasema kuwa mbunge wa jimbo hilo yupo pamoja nao huku akisisitiza kuwa kama kauli mbiu ya sherehe za Uhuru inavyotaka wananchi kufanya kazi, Mbunge amejipanga kupiga kazi kwelikweli kwa kushirikiana na halmashauri ya manispaa ya Ilemela, chama cha mapinduzi, ofisi ya mkuu wa wilaya, madiwani na wananchi wote kwa ujumla ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana na nchi inasonga mbele kwa haraka ili kutimiza kiu ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuhakikisha wananchi hasa wanyonge wanatatuliwa kero zao na kupata maendeleo.
Nae katibu wa umoja wa vijana wa chama hicho kwa wilaya ya Ilemela UVCCM, Ndugu Nehemia Philemon mbali na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli kwa kuyaishi maono ya Uhuru kwa kuhakikisha nidhamu inakwepo kwa wafanyakazi, umoja, uzalendo na mshikamano unadumishwa baina ya wananchi akamshukuru mbunge wa jimbo hilo na madiwani kwa ushirikiano wanaoutoa kwa vijana na chama huku akiwataka vijana kuziishi ndoto za wapigania uhuru.