Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akisalimiana na Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha alipowasili katika ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia kadi aliyopewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo baada ya kumalizika kwa kikao cha Menejimenti ya Wizara kilichoongozwa na Waziri wa Ardhi William Lukuvi (kulia) walipowasili katika ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akisisitiza jambo wakati wa kikao na Menejiment ya Wizara ya Ardhi alipowasili kwa mara ya kwanza katika ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020. Wengine ni Naibu wake Dkt Angeline Mabula (wa pili kulia), Katibu Mkuu Mary Makondo (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Zakaria Kerra (wa kwanza kushoto)
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi na Naibu Wake wakisalimiana na watumishi wa Wizara ya Ardhi walipowasili katika ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma leo tarehe 10 Desemba 2020. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
**************************************
Na Munir Shemweta, WNMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kujipanga upya kwa kuwa wabunifu katika utekelezaji majukumu na kusisitiza kwamba hatomvumilia mtendaji atakyeshindwa kutekeleza majukumu yake.
Aidha. Alisema katika kuhakikisha utendaji wa sekta ya ardhi unaleta mafanikio katika mikoa nchini atamtuma Naibu wake Dkt Angeline Mabula kufanya ukaguzi maalum wa ofisi za ardhi za mikoa ili kuangalia kazi zilizotekelezwa tangu kuanzishwa ofisi hizo.
Akizungumza na Menejimenti Wizara leo tarehe 10 Desemba 2020 jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuapishwa hapo jana, aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kujipanga upya na kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ushirikiano na kusisitiza kuwa watumishi wa wizara hiyo wakishirikiana vizuri wanaweza kufanya mambo mengi na makubwa zaidi.
‘’Kuna mambo katika awamu iliyopita tulitakiwa tuyafanye lakini hayakufanyika safari hii hatutakubali kurudi nyuma, nataka niondoke katika wizara hiyo kwa heshima’’ alisema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi aligusia pia sekta ya uwekezaji aliyoieleza kuwa Wizara yake inatakiwa kuifanyia kazi kwa umakini ikiwemo kuwa na kumbukumbu sahihi za uwekezaji uliofanyika nchini, faida yake kwa taifa na kama ulisaidia kwa kiasi gani kutoa jiara kwa watanzania.
Aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwa na takwimu za taarifa zote za msingi katika wizara na kutolea mifano ya taarifa za hati zilizotolewa, maeneo yaliyopimwa pamoja na maeneo ya uwekezaji katika mashamba na faida yake na kusisistiza msingi wa uwekezaji unaanzia Wizara ya Ardhi.
‘’Ni lazima tujitayarishe kwa kuwa matajiri wa takwimu na taarifa za msingi katika maeneo yetu kwani inakera kusikia hakuna takwimu katika eneo fulani ‘’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi yeye pamoja na Naibu wake hawakurudishwa kwenye wizara hiyo kwa bahati mbaya na wanataka kufanya kazi maradufu ili kuondoka na rekodi ya kishindo katika utendaji kazi wa wizara hiyo.
Akigeukia Ofisi za Ardhi za mikoa Lukuvi alisema, baada ya wizara kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa sasa kinachofuata ni Wizara hiyo kufanya tathmini kwa kuangalia utendaji kazi wa ofisi hizo kama una tija na ulikuwa sahihi.
‘’Nataka kuona kila ofisi imefanya nini tangu kuanzishwa kwake na kila kamishna wa Ardhi Msaidizi katika mkoa atupatie taarifa yake amefanya nini tangu kuanzishwa kwa ofisi yake’’ akisema Lukuvi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, Wizara ya Ardhi ina kazi kubwa ya kuhakikisha inatimiza lengo lake la makusanyao ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200.
Aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanajikita katika kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi na kupongeza ubunifu ulioanzishwa na Wizara kutoa elimu kwa wamiliki wa ardi kila mwishoni mwa wiki.
Akizielezea sula la maashamba pori, Dkt Mabula alisema pamoja na kazi kubwa kufanyika ya kufanya ukaguzi wa mashamba pori lakini kunahitajika kazi ya haraka na kuchukua hatua kwani kazi bado ndefu katika suala hilo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo William Lukuvi na Naibu wake Dkt Angeline Mabula ndiyo mawaziri pekee waliorejeshwa katika wizara moja tofauti na wizara nyingine ambapo aidha alibaki waziri ama naibu waziri.