Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William (kulia) akielezea jinsi wawekezaji wa Wilaya ya Munfindi wanavyoweza kunufaika na fursa za uwekezaji zilizopo Jiji la Dodoma kwa timu ya kimkakati ya masoko kutoka Jiji la Dodoma. Timu hiyo ilipomtembelea ofisini wake wiki mapema wiki hii.
******************************************
TIMU ya kimkakati ya masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekaribishwa wilayani Mufindi kuvutia wawekezaji kwenda kuwekeza jijini Dodoma na kukuza uchumi wa taifa.
Ukaribisho huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri Willian alipokutana na kufanya mazungumzo na timu ya kimkakati ya masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofika kumsalimia ofisini kwake mjini Mafinga.
William alisema “mimi niwakaribishe sana Mufindi kuangalia fursa za uwekezaji kwenye wilaya yetu kwa sababu wawekezaji wakiwekeza Jiji la Dodoma wanakuwa wamewekeza Tanzania, wakiwekeza Mufindi wanakuwa wamewekeza Tanzania. Najua uwekezaji unategemea sana vivutio vilivyopo eneo husika”.
Akiongelea dhana ya uwekezaji, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa uwekezaji ni ushirikiano wa pande zaidi ya moja. “Katika uwekezaji tunategemeana, sisi tunajitahidi kuvutia wawekezaji Mkoa wa Iringa, lakini uwekezaji unakuwa kwenye mnyororo wa thamani. Sisi zao letu kubwa Mufindi ni mbao na bidhaa zinazotokana na misitu. Tunatengeneza bidhaa za misitu na ndiyo maana tuna viwanda vingi vya mazao ya misitu. Tunakiwanda kikubwa cha karatasi na malighafi mkubwa ni mbao” alisema William.
Aidha, alisema kuwa zikipigwa hesabu za kiuchumi, tayari kuna wawekezaji wa Mufindi ambao wamewekeza Jijini Dodoma. Alikitolea mfano kiwanda cha Sao Hill ambacho kina tawi jijini Dodoma wakipasua na kutibu mbao.
Akiongelea fursa ya hali ya hewa ya Mufindi kwa kilimo cha mbogamboga na uwekezaji katika Jiji la Dodoma, Mkuu huyo wa Wilaya alisema “sisi kwa hali ya hewa tuliyonayo, tunaweza kuzalisha matunda na mbogamboga na kuziuza jijini Dodoma mwaka mzima. Hivyo, hii ni fursa ya kuwekeza katika eneo hilo. Nafahamu kuwa Serikali inajenga uwanjwa mkubwa wa kimataifa wa Ndege wa Msalato utakaowezesha hata kusafirisha nje ya nchi mbogamboga na matunda kutoka Mufindi”.
Akimuelezea fursa za uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Maendeleo ya Jamii katika Jiji hilo, Zainab Manyike alisema kuwa Jiji hilo limepima na kutenga viwanja vya matumizi mbalimbali katika maeneo tofauti.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepima viwanja vya viwanda katika Kata ya Nala, eneo hilo vinaweza kujengwa viwanda vya kuchakata mazao ya misitu. Hii ni fursa kwa wananchi wa wilaya Mufindi kuwekeza jijini Dodoma. Aliongeza kuwa wawekezaji wa wilaya ya Mufindi wanaweza kujipanga kunufaika na ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa Msalato Jijini Dodoma ili kuweza kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga ndani na nje ya nchi” alisema Manyike.