******************************
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeadhimisha siku ya maadili kwa kusikiliza kero za wananchi Vijijini.
Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Simanjiro, Adam Kilongozi ametoa elimu ya rushwa na kusikiliza kero za wananchi kwenye Kijiji cha Oiborkishu Kata ya Oljoro namba tano.
Kilongozi amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na dhuluma bila kutishwa na mtu yeyote.
Amesema hivi karibuni wananchi wa eneo hilo walitoa malalamiko yao TAKUKURU kwamba wanachangishwa michango bila kupewa risiti.
Mmoja kati ya wananchi wa eneo hilo Robert Mollel ameipongeza TAKUKURU kwa kufuatilia suala hilo kwani wananchi walikuwa wanachangishwa michango bila kupewa risiti.
Amesema baada ya kutoa taarifa TAKUKURU juu ya kitendo hicho hatua za haraka zimechukuliwa hivyo wananchi kuwa na imani na serikali yao.