Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote katika kuadhimisha Kampeni ya Kimataifa inayojulikana zaidi kwa jina la Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto Duniani ikiwa na kauli mbiu inayosema: “Tupinge Ukatili wa Kijinsia: Mabadiliko Yanaanza na Mimi”. Kampeni hii huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 25 Novemba na kufikia kilele chake tarehe 10 Disemba.
Kampeni hii ilianzishwa kwa mara ya kwanza na Taasisi ya “Women’s Global Leadership” (WGL) mwaka 1991 katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani ambapo hadi kufikia sasa zaidi ya mashirika 6,000 kutoka takribani nchi 187 yanaendelea kushiriki katika kampeni hii. Siku hii ilitambulika rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 1999.
Lengo la kuwepo kwa siku hizi ni kuhamasisha jamii kulinda, kuhifadhi, kutetea na kuheshimu haki za wanawake na watoto. Siku hizi pia zina lengo la kusaidia kuijengea jamii uelewa mpana kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya wanawake na watoto na namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Tume inapenda kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada mbalimbali zilizochukua katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuanzisha Mipango Mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto Tanzania Bara na Zanzibar. Mipango hii imelenga kupunguza ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa. Pia kuwepo kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi ambapo madawati 420 yameanzishwa. Madawati haya yamewezesha wahanga 58,059 kufikiwa na kupatiwa huduma.
Jitihada nyingine ni kuanzishwa kwa vituo 12 vya Mkono kwa Mkono (One Stops Centres) vya kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia pamoja na kamati 11,520 za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya kitaifa.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali, Tume inatambua kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika kujenga jamii salama isiyo na vitendo vya ukatili wa kijinsia. Baadhi ya changamoto hizo ni mila, desturi na imani zinazoruhusu watoto wa kike kuolewa katika umri mdogo badala ya kuendelea na masomo. Aidha, mila za ukeketaji watoto wa kike pamoja na rushwa ya ngono katika maeneo ya kazi na vyuo vikuu ni kikwazo katika kufanikisha juhudi hizo za Serikali.
Hivyo basi, Tume inaisihi jamii kuacha mila, imani na desturi potofu ambazo ni chachu ya kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Tume inatoa msisitizo kwa watumishi wa umma na mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia na kuheshimu kanuni na taratibu za maadili ya utumishi wa umma ili kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu, Tume inawasihi wananchi kutokuyafumbia macho matukio kama hayo yanapotokea katika jamii zetu na kutoa taarifa kwa wakati katika mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe.
Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, Tume inategemea kufanya makongamano ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), Dar es Salaam na Zanzibar ili kuwajengea uelewa wanajumuiya na hasa wanachuo kuhusu haki za binadamu na namna ya kuondokana na vitendo vya ukatili katika mazingira walimo. Tume itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu kupitia vipindi vya redio.
Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wote katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili katika jamii zetu vinakomeshwa na haki za binadamu zinaheshimiwa na kulindwa na kila mmoja wetu.