*******************************************
Na Mwandishi wetu- Chamwino- Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeadhimisha Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri kwa kupanda miti na kufanya usafi Wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo Desemba 9, 2020.
Akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu lengo la mpango huo, Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Kanali Hassan Mabena amesema kuwa upandaji miti katika hospitali ya Uhuru ni moja ya shughuli zilizopangwa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi wa Chamwino ikiwa ni moja ya hatua za kutunza mazingira katika kuadhimisha siku ya Uhuru..
“ Tumepanda miti 400 katika eneo hili la hospitali ya Uhuru ambayo ujenzi wake tayari umefikia asilimia 97 na asilimia 3 zilizobaki tutahakikisha tunazikamilisha kufikia Desemba 15,2020 ili huduma zianze kutolewa kama agizo la Serikali linavyotaka”,alisisitiza Kanali Mabena.
Akifafanua, amesema kuwa kujengwa kwa hospitali hiyo kutasaidia kuimarisha huduma za afya katika eneo la Chamwino ambapo pia alishushukuru Serikali kwa kuwaamini JKT kutekeleza mradi huo ambao utakamilika kama ilivyopangwa.
Aliongeza kuwa kazi zinazoendelea ni za kumalizia masuala madogo yaliyobaki na pia wanatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi wa uzio ili hospitali hiyo ianze kutoa huduma.
Naye, Mkuu wa Kambi, Kikosi cha Makao Makuu ya JKT Luteni Kanali Alex Malenda amesema kuwa shughuli nyingine iliyofanyika ni kufanya usafi katika Kituo cha Afya Chamwino kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru na 58 ya Jamhuri.
Aidha, kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Yustina Amo amesema kuwa wanashukuru JKT kwa kufanya usafi katika Kituo cha Afya Chamwino.
Aliongeza kuwa jamii inapaswa kuiga mfano bora unaooneshwa na Jeshi la Kujenga Taifa katika kufanya usafi na kutunza mazingira.
Kwa upande wake Mzee Peter Mavunde aliyeshiriki pamoja na Maafisa Wakuu,Maafisa na Askari wa JKT katika zoezi la kupanda miti katika hospitali ya Uhuru ameipongeza JKT na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujenga hospitali hiyo na miradi mingi mikubwa ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.