Mkuu wa wilaya Biharamulo Kanali Mathias Kahabi wapili kushoto pamoja na mbunge wa jimbo la Biharamulo Mhe. Mhandisi Ezra Chiwelesa watatu kushoto wakiangalia hali halisi ya wananfuzni katika shule ya msingi Busiri wananvyosoma.
Mkuu wa wiaya Biharamulo Kanali Mathias Kahabi akiwahubia wananchi wa kijiji cha Busiri wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi desemba 08,2020
Muonekano wa shule ya msingi Busuri yenye vyumba vya madarasa viwili pamoja na ofisi moja ya walimu ikibeba wananfunzi 350 kuanzia darasa la kwanza hadi la nne.
Mhe.Mhandisi Ezra John Chiwelesa mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi akiongea na wananchi wa kijiji cha Busiri wakati wa ziara ya kusikiliza kero za wananchi desemba 08,2020.
Wanafunzi wakishushwa kwenye semi baada ya kupewa lifti wakitokea shuleni.
**************************************
Biharamulo – Na Allawi Kaboyo.
Wanafunzi 350 kuanzia darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Busiri iliyopo kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo wanalazimika kutumia vyumba viwili vya madarasa kutokana na ujenzi wa vumba hivyo kukwama baada ya wananchi kugoma kuendelea kuchangia kwa kigezo cha kutojua matumizi ya fedha wanayoichanga.
Wakiwa kwenye ziara ya kusikiliza kero za wananchi desemba 08, mwaka huu, viongozi hao wamefika katika shule hiyo na kujionea halihalisi ya namna wananfunzi hao wanavyosoma huku shule nzima ikiwa haina madawati na kuwalazimu wanafunzi hao kukaa chini.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo mwalimu mkuu, mwalimu Stephano Raphael amesema kuwa shule hiyo inazo changamoto nyingi ikiwemo Madawati, Vyumba vya madarasa,vyoo vya wanafunzi ambapo ameeleza kuwa wananfunzi hao wanalazimika kutumia matundu mawili ya vyoo hali inayowapelekea kuishi kwa tabu sana.
Akiongea na wanafunzi pamoja na wwalimu shuleni hapo, mkuu wa wilaya ya Biharamulo Kanali Mathias Kahabi ameupongeza uongozi wa shule kwa kuendelea kuwafundisha wanafunzi japo kwa mazingira magumu na kuwaahidi kuwa changamoto hizo zinakwenda kumalizika muda sio mrefu.
“Wakati wa kampeini wananchi walimsimamisha Mhe. Waziri mkuu hapa alipokuwa akitokea Ngara na kumueleza suala la shule hii ambayo awali ilikuwa na walimu watatu tena wa kujitolea, maelekezo yalitolewa hapo hapo na walimu wakaletwa wanne sasa niwaombe wanangu vumilieni kwenye kipindi hiki kifupi hizi changamoto tutazimaliza ndio maana nimekuja hapa pamoja na mbunge.” Amesema Kanali Kahabi.
Katika mkutano wa hadhara na wananchi, Mbunge wa jimbo la Biharamuo Magharibi Mhe. Mhandisi Ezra Chiwelesa amewashukuru wananchi hao kwa kuanzisha ujenzi wa shule hiyo baada ya kuona watoto wao wakishindwa kusoma kutokana na shule kuwa mbali ya zaidi ya kilometa 18 na kuwapelekea watoto hao kukosa muelekeo wa maisha.
Ezra amesema kuwa kijiji hicho ambacho kipo kwenye maeneo ya machimbo ya madini ya Dhahabu haiwezekani wananchi washindwe kujenga shule kwaajili ya watoto wao na kuwataka wananchi hao kueleza tatizo ni nini hadi ujenzi umekwama kuendelea.
“Nyinyi ni wazazi na wanaotakiwa kusoma hapa ni watoto wenu haiwezekani mkashindwa kuendeleza ujenzi huu, kuna msingi wa vyumba 6 ambao umesimama kwa takribani miaka 5 hebu tuelezeni shida ni nini? Kama kuna tatizo tumekuja sasa kulimaliza maana watoto wanatia huruma na kwa serikalihiiya awamu ya 5 hatuwezi kuruhusu hali hiyo ikaendelea.” Amesema Mbunge Ezra.
Wakitoa kero walizonazo baadhi wananchi hao wengi wao wamekuwa wakisumbuliwa na migogoro ya ardhi ambayo imesababishwa na viongozi wa kijiji hicho kwa kuwanyang’anya ardhi zao na kuwauzia watu wenye fedha huku wengine wakiwa wamedhurumiwa kabisa.
“Tumepoteza watoto wengi hapa hasa wa kike kwa kupata mimba na wengine kuolewa, wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kwenda kutafuta shule na huko wanakutana na watu wanaoedesha masemi ambao wamekuwa wakiwabeba kwa lengo la kuwa lifti na wengine wameishia darasa la nne kwa kushindwa kumu mwendo wa kwenda shuleni zaidi ya kilomita 18” amesema mmoja wa wanakijiji.
Kuhusu mkwamo wa shule wananchi hao wamesema kuwa wamekatishwa tama na viongozi wa kijiji akiwemo mtendaji wa kijiji pamoja na mwenyekiti wa kijiji kwa kuwachangisha michango ya ujenzi wa shule bila kuwasomea mapato na matumizi lakini wakihoji wanaambiwa makaratasi ya kumbukumbu ya michango yamepotea.
Alipoulizwa kuhusu suala la kusoma taarifa ya mapato na matumizi mtendaji wa kijiji hicho Omary Ramadhan amejibu kuwa anakumbukumbu za watu ambao hawajalipa huku mwenyekiti wa kijiji hicho akisema kuwa kumbukumbu za waliochangia hazipo.
Mara baada ya kusikiliza hoja hizo viongozi hao waliwatia moyo wananchi na kuwaeleza kuwa utatengenezwa utaratibu mzuri wa uchangiaji na kuwahakikishia kuwa hakuna pesa yao ambayo italiwa na badala yake itatumika kuwaletea maendeleo ambapo mkuu wa wilaya aliamua kuondoka na mwenyekiti pamoja na mtendaji kwaajili ya mahojiano zaidi.