********************************
Na Woinde Shizza ,Arusha
Spika wa bunge la jamuhuri la muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuomba mkuu wa Chuo cha Uhasibu Prof.Eliaman Sedoyeka pamoja na utawala kuongeza juhudi za ujenzi wa tawi jipya la chuo hicho ili watanzania wengi wanufaike na mafunzo yanayotolewa.
Akizungumza katika mahafali ya 22 ya chuo hicho yaliyofanyikia wilayani Arumeru,Spika Ndugai alisema tawi la chuo hicho likijengwa jijini Dodoma kitasaidia hata waheshimiwa wabunge katika kujifunza masuala yahusuyo uongozi na utawala.
“Kama ambavyo chuo cha uhasibu kimejipanga kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali kuhusu masuala ya uongozi na utawala hivyo napenda kuwaase nyinyi mnaohotimu kutumia elimu mliyoipata katika kufanya kazi za ubunifu ambazo zitasaidia kukuza uchumi wenu na nchi kwa ujumla,”alisema Spika Ndugai.
Spika Ndugai alisema katika kipindi hiki elimu imekuwa ni ukombozi,ni gharama kwani serikali imeweka fedha nyingi katika elimu ili kuhakikisha wanaipata ikiwa hata wazazi,walezi pia wamegharamia hivyo wanayo matarajio ya wahitimu hao kutumia elimu walionayo katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Prof.Sedoyeka alisema chuo hicho kimekuwa kikiwafundisha wanafunzi wake katika kujitengenezea ajira pamoja na kuwasaidia kuendeleza mawazo yao ya kibiashara ili kuweza kukuza biashara kwani kufanya hivyo kutamsaidia kujiajiri na kuajiri wengine.
“Katika kufanya hivyo kutaongeza pato la Taifa na dhana ya uchumi wa kati kutaendana na uzalishaji mali hivyo chuo kinaendelea kuboresha mitaala ya ufundishaji katika wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi na mwaka ujao wataanzisha mtaala wa utalii ,posta pamoja na ujasiriamali,”alisema Prof.Sedoyeka.
Hata hivyo Mkuu huyo alisema kuhusu ombi la Spika Ndugai amelipokea kama maelekezo na watakwenda kufanyia kazi kwani Dodoma tayari wanaeneo la ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa chuo lenye square mita takribani 24000 na sasa wanampango ikiwa January 2021 wataanza utaratibu wa ujenzi.
alisema sasa hivi wanashughulikia vibali vya ujenzi lakini ni mpango mkakati wao wa kwenda Dodoma nakuonyesha hali halisi ya makao makuu ya nchi kwa kuanzisha tawi jipya la chuo hicho kwani mitaala yao ya uongozi na utawala umekuwa ukifanya vizuri katika kuwafua viongozi pamoja na mitaala mingine.
Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai akikabidhi cheti cha pongezi kwa mhitimu aliyefanya vizuri katika mahafali ya 22 chuo Cha Uhasibu Arusha iliyofanyika katika hotel ya kitalii ya Ngurudoto, iliopo ndani ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha juzi katikati ni Mkuu wa chuo hicho Prof Eliaman Sedoyeka (picha na Woinde Shizza ,ARUSHA).