Mashamba ya miti ya mitiki mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma
***************************************
Programu ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC) imetoa ruzuku ya miche ya mitiki zaidi ya 81,000 iliyopandwa katika hekta 72.1 kwa wakulima 80 mwambao mwa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma msimu wa mwaka 2019/2020.
Mwenyekiti wa Muungano wa Chama cha Wazalishaji wa miti ya misaji (mitiki) kijiji cha Liuli wilaya ya Nyasa Samwel Mawanja amesema FORVAC wanaendelea kufadhili mradi wa miti ya mitiki ambayo inatekelezwa katika vijiji sita mwambao mwa ziwa Nyasa.
“Katika msimu wa mwaka 2020/2021 tumeomba tena FORVAC ruzuku ya miche ya mitiki 300,000 kupitia vijiji sita vinavyozalisha mitiki ambavyo ni Liuli,Nkalachi,Nkali A,Nkali B na Lipingu na Hongi’’,alisema Mawanja.
Amesema mradi wa mitiki ni mradi pekee ambao haujawahi kutekelezwa tangu uhuru mwambao mwa ziwa Nyasa ambao unatarajia kuleta tija kubwa kiuchumi kwa wananchi hivyo kuleta mapinduzi makubwa kiuchumi baada ya miti hiyo kuanza kuuzwa.
Ameyataja matarajio ya wananchi hao ambao pia ni wavuvi katika ziwa Nyasa kuwa ni kutengeneza boti za kisasa kwa kutumia miti ya mitiki zitakazowawezesha kwenda kuvua mbali badala ya kuendelea kuharibu misitu ya asili kwa kukata miti ya kutengenezea mitumbwi.
Kwa upande wake Mratibu wa FORVAC Taifa Emanuel Msoffe akizungumza baada ya kukutana na kikundi hicho cha wazalishaji mitiki,ametoa rai kwa wananchi mwambao mwa ziwa Nyasa kulinda na kuhifadhi misitu iliyopo kwenye milima ya Livingstone kwa kuacha kulima na kukata miti hovyo.
Amesisitiza kuwa eneo la Mwambao mwa ziwa Nyasa linafaa sana kwa uzalishaji wa mitiki kwa sababu ni eneo ambalo lipo chini ya milima ya livingstone hivyo lina rutuba nyingi.
“Natoa rai kwa wananchi mwambao mwa ziwa Nyasa kuendelea kupata miti ya mitiki kwa sababu kati ya miaka 15 hadi 20 mtavuna na kupata fedha nyingi zitakazobadilisha kabisa maisha yenu’’,alisisitiza Msoffe.
Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya Nyasa Bugingo Bugingo amesema utafiti umebaini kuwa hekari moja ya mitiki inaweza kumuingizia mkulima zaidi ya milioni 400 hivyo ni muhimu wananchi kupanda miti hiyo ili kukuza uchumi wao.
Bugingo anayataja miongoni mwa matumizi ya zao la mitiki ni kutengenezea vitako vya silaha aina ya bunduki,vyombo vya majini kama vile meli na boti na kutengeneza samani mbalimbali zenye gharama kubwa.
Utafiti umebaini kuwa Mahitaji ya mtiki katika soko la duniani ni makubwa ,ndiyo maana nchi za Ulaya na nchi za Asia zikiongozwa na China na India wananunua miti aina ya mitiki kwa wingi kutoka Tanzania,na hata hatujaweza kufikisha hata robo ya mahitaji yao.
Nchi ya Malyasia kwa mwaka hupata mapato ya Dola za Marekani zaidi ya bilioni 13 kutokana na kilimo cha mitiki.Mahitaji ya soko la mitiki ni makubwa hivyo wakulima wapya wa mitiki katika wilaya ya Nyasa na maeneo mengine nchini waongeze uzalishaji wa zao hili, mahitaji yake yanaendelea kuongezeka