Soko la mnada wa zao la ufuta katika kituo cha Lilambo wilayani Songea ambalo limefanyika hivi karibuni.
************************************
Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imegawa mbegu ya ufuta bure kwa wakulima wa zao la ufuta katika Kata ambazo zinazalisha zao hilo kwa wingi kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020 /2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri hiyo Bw Simon Bulenganija amesema ametumia kiasi cha sh. milioni 10 kwa ajili ya kununua mbegu hiyo kwa lengo la kuwasaidia wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji kutoka gunia tatu hadi tano kwa ekari moja,tofauti na awali wakulima walikuwa wakizalisha gunia moja hadi tatu kwa ekari moja kwakutuia mbegu ya kienyeji.
Ametaja idadi ya kilo zilizonunuliwa na kusambazwa kwa wakulima kuwa ni kilo 1000 na aina ya mbegu ni Lindi 02 zilizonunuliwa kutoka Kituo cha Utafiti wa Mazao cha Naliendele kilichopo Mkoani Mtwara.
Amezitaja kata na idadi ya kilo zilizosambazwa kuwa ni kata Muhukuru Barabarani na Lilahi ambao wamepata kilo 225,Kata ya Matimira kilo 180,Kilagano kilo 180,Kizuka 180,Ndongosi kilo 90 na Magagura kilo 90.
Bulenganija ameyataja malengo ya kusambambaza mbegu hiyo ni kuwapunguzia wakulima gharama ya kununua mbegu ya ufuta ambayo huuzwa shilingi 10,000 kwa kilo moja pia kuongeza uzalishaji na Serikali iweze kupata mapato kupitia ushuru unaotolewa na wakulima mara baada ya kuuza kupitia vyama vyao vya ushirika.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Mazao wa Halmashauri hiyo Norbert Rugonza amewashauri wakulima wa zao la ufuta wasitegemee matokeo chanya kwenye kilimo bila kusimamia vizuri na kufuatilia wakati wa uzalishaji.
Amesema wakulima ambao wamebahatika kupata mbegu hizo wanatakiwa kuzitumia kama shamba darasa kwakuzalisha kwa wingi na kusambaza kwa wakulima wengine kwenye msimu wa kilimo wa mwaka 2021 /2022.
Amesema mbegu ya aina ya lindi 02 ni mbegu bora na nzuri kwa kilimo cha ufuta kwa sababu ni mbegu ambayo inastahimili magonjwa hivyo ni vema wakulima wakaachana na dhana potofu ya kwamba mbegu za kisasa zina matatizo ya kushambuliwa na magojwa na wadudu jambo ambalo halina ukweli.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Shekiel Masawe amesema katika msimu wa mwaka 2018/2019 ilifanikiwa kuzalisha zao la ufuta kilo milioni 1,316,227 na katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 ilizalisha zao la ufuta kilo milioni 2,378,172 na kufanikiwa kuingiza mapato ya Zaidi ya shilingi milioni 400.