*********************************
NJOMBE
Diwani wa kata ya Uhenga alieshinda katika uchaguzi mkuu kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo chadema Alfan Kawambwa ameungana na madiwani wengine 27 wa chama cha mapinduzi kula kiapo cha uadilifu cha kuwatumikia wakazi wa jimbo la Wanging’ombe katika kipindi cha miaka ijayo.
Kawambwa amekula kiapo ikiwa bado chama chake hakija weka bayana kama kinatoa ruhusa kwa wawakilishi wake wa ngazi ya Ubunge na Udiwani kuendelea na majukumu ya kiserikali ya uwakilishi katika bunge na baraza la madiwani na kwamba amelazimika kula kiapo kwa kuwa hakuna barua ya katazo amepewa na chama hivyo anakwenda kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi waliokiamini chama chake.
Wakati historia ikiandikwa kwa mara ya kwanza kwa jimbo la Wanging’ombe kupata diwani mmoja wa upinzani, madiwani wa chama cha mapinduzi jimboni humo akiwemo Onesmo Lyandala,Anaupendo Gombela na Thobias Mkane wanasema mchanganyiko wa vyama utalifanya baraza hilo kuwa bora zaidi na kuahidi kumpa ushirikiano diwani wa upinzani kwa maslahi ya wakazi wa Wanging’ombe
Akitoa Salamu za serikali kuu katika baraza hilo lililoambatana na uchaguzi wa Mwenyekiti,Makamu mwenyekiti na kamati za madiwani,mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Lauteri Kanoni ameanza kwa kumpongeza diwani wa upinzani kwa kushindi na kisha kutoa agizo la kuanza mapambano ya mimba mashuleni,Kuanza Mchakato wa ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya wilaya pamoja na kutenga siku za kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Katika Agenga ya Uchaguzi wajumbe wote wamechagua Agnetha Mpangile kuwa mwenyekiti na Onesmo Lyandala kuwa makamu mwenyekiti ambao kwa nyakati tofauti wameahidi kupigania maslahi ya umma zaidi kuliko matumbo yao.