Mgombea na nafasi ya uenyekiti wa Shirikisho hilo David Msuya akizungumza na waandishi wa habari hii leo katika ofisi za BMT Jijini Dr es Salaam. Afisa uhusiano wa BMT Frank Mdunga akizungumza na waandishi wa habari hii leo katika ofisi za BMT Jijini Dr es Salaam.
*******************************
IKIWA zimebaki siku chache kabla ya dirisha la zoezi la uchukuaji fomu wa kugombea nafasi mbalimbali katika Chama cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA,) Mgombea na nafasi ya uenyekiti wa Shirikisho hilo David Msuya amehaidi kujenga ofisi ya michezo ya asili katika kila Wilaya ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuuenzi utamaduni wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurudisha fomu hiyo katika ofisi za BARAZA la Michezo Tanzania (BMT,) leo jijini Dar es Salaam, Msuya amesema amegombea nafasi hiyo ya uenyekiti kwa kuwa ni mwanamichezo kamili na anayeipenda fani hiyo.
“Nimesoma TASUBA…naelewa sekta hii ilivyo na ninauzoefu nayo kinachotakiwa na ushirikiano katika kuhakikisha utamaduni wa mtanzania unafahamika kitaifa na ulimwengu kwa ujumla.” Amesema.
Msuya amesema, Licha ya kuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Furahika Education College amekuwa akishiriki kwa karibu shughuli za michezo kwa kugawa vifaa mbalimbali kwa shule za jijini humo kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Amesema endapo atapata nafasi hiyo atahakikisha utamaduni wa mtanzania unakuzwa kuanzia ngazi elimu ya msingi kwa kufundisha wanafunzi na hiyo yote ni katika kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais Dkt.John Joseph Magufuli ambaye amekuwa mbeba maono mema kwa watanzania.
Kwa upande wake Afisa uhusiano wa BMT Frank Mdunga amesema, wenye sifa za kugombea nafasi hizo wajitokeze kabla ya Desemba 13 mwaka huu ili waweze kupata nafasi ya kuendeleza michezo ya jadi nchini.
Amesema uchaguzi mkuu wa nafasi zinazogombewa utafanyika Desemba 19 mwaka huu na utatanguliwa na kampeni na hiyo yote ni katika kuhakikisha Taifa linaendelea mbele katika michezo ya jadi.
Aidha amesema kuwa hadi sasa ni wagombea wawili pekee ndio waliorudisha fomu na mmoja kuirejesha na amewataka wenye vigezo ikiwemo kuwa mtanzania, mwanamichezo, asiyewahi kukutwa na makosa ya jinai bila kuzingatia ngazi ya elimu anaweza kuwania nafasi hizo.
Nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo ni Mwenyekiti, makamu mwenyekiti, Katibu, Kaimu Katibu, mhazini na nafasi nne kwa wajumbe.