Sehemu ya jengo la kiwanda cha kutengeneza vifungashio kinachojengwa na Chama kikuu cha Ushirika cha Sonamcu kwa gharama ya zaidi ya bilioni 1.2 ambacho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza vifungashio vitakavyotumika kwa wakulima na wajasirimai wadogo wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma,
********************************
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
CHAMA kikuu cha Ushirika wilaya ya Namtumbo na Songea(Sonamcu) mkoani Ruvuma, kimeanza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha vifungashio kama mkakati wa chama hicho kuwaondoa usumbufu wanachama wake kutafuta vifungashio kutoka viwanda vingine gharama kubwa na kama sehemu ya chanzo cha mapato.
Meneja Mkuu wa Sonamcu Juma Mwanga amesema, kiwanda hicho kinajengwa katika wilaya ya Namtumbo na kazi inaendelea kwa kasi kwa ghrama ya zaidi ya bilioni 1.2 zitakotolewa na benki ya maendeleo ya kilimo nchini ambapo lengo ni kuwahi msimu wa mavuno 2021.
Alisema, mara baada ya ujenzi wa kiwanda kukamilika, itafungwa mitambo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha vifungashio na hivyo kuwaondolea kero wanachama wa chama hicho ambao wakati mwingine wanalazimika kuagiza vifungashio mkoani Dar es salaam na maeneo mengine hapa nchini.
Alisema, kwa sasa wameanza kujenga kiwanda hicho kutoka fedha za mapato yake ya ndani wakati wanasubiri fedha nyingine kutoka benki ya kilimo Tanzania(TADB) ambazo zitatumika kununua mitambo na kukamilisha ujenzi wake.
Alisema, kimsingi kiwanda kitakapokamilika na kuanza kazi kitasaidia sana kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na bidhaa za wajasirimali wadogo kama vile wasindikiji ambao wanalazimika kutumia vifungasho visivyo na ubora na hivyo kushusha thamani ya bidhaa pindi wanapofikisha kwa walaji.
Mwanga alisema, vifungashio vitakavyotengenezwa katika kiwanda hicho kwa kiasi kikubwa ni vile vitakavyotumika kwa zao la tumbaku linalolimwa na wanachama wa Sonamcu kutokana na mahitaji kuwa makubwa.
Aidha alisema,mbali na vifungashio kwa zao la tumbaku kiwanda kitakuwa na uwezo wa kutengeneza vifungashio vya mazao mengine hasa ikizingatia kuwa mkoa wa Ruvuma ni maarufu kwa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara na kitakuwa kiwanda cha kwanza cha vifungashio mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa Mwanga,vifungashio vitakavyotengenezwa pia vitapelekwa katika vyama vingine vya ushirika kama (Tamcu Ltd) cha Tunduru kwa ajili ya zao la korosho na chama kikuu cha Ushirika Mbinga (Mbifacu) ambacho kimejikita zaidi katika zao maarufu la kahawa.
Afisa ushirika wa wilaya ya Namtumbo Emmanuel Gwao amekipongeza chama kikuu cha ushirika Sonamcu kwa uamuzi wa kujenga kiwanda hicho wilayani Namtumbo kwani wakulima watakuwa na uhakika wa kupata vifungashio vya mazao yao.
Alisema, ujenzi wa kiwanda hicho ni kama kulipa fadhila kwa wana Namtumbo kutokana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia 90 ya vyama vya msingi vya ushirika vinavyolima zao la Tumbaku mkoani Ruvuma viko katika wilaya hiyo.
Pia alisema, kujengwa kwa kiwanda hicho kutainufaisha jamii ya watu wa Namtumbo kupata ajira katika kiwanda hicho na itakuwa fursa kubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji kwani wana uhakika wa kupata vifungashio bora vya mazao wanayozalisha.
Alisema, halmashauri nayo itanufaika kwa kupata fedha kodi ya huduma kutoka kwenye kiwanda na hivyo halmashauri itaweza kujiendesha kutokana na mapato yake ya ndani na kuwataka wakulima ambao ni wanachama wa chama hicho kuongeza uzalishaji wa tumbaku na maazao mengine yanayostawi vizuri katika wilaya hiyo.
Alisema, hiyo ni fursa pekee kwa wakulima wa Namtumbo na Ruvuma badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya mkoa sasa bidhaa hizo zitapatikana katika wilaya hiyo na kuwaomba wajasiriamali wadogo kutumia fursa hiyo kutengeneza bidhaa bora.
Pia, ameyaomba makampuni na watu binafsi kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo ambayo kuna fursa nyingi za uwekezaji kama ardhi nzuri na Amani na utulivu ikilinganisha na maeneo mengine hapa nchini ambako mwekezaji anapotaka kuwekeza ni lazima apitie mlolongo mrefu.
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo Aden Nchimbi ameipongeza Sonamcu kutokana na shughuli wanazozifanya katika wilaya hiyo hasa shughuli za wakulima ambapo katika miaka miwili zaidi ya bilioni 50 zimeingizwa kwa wakulima wa wilaya hiyo.
Alisema, kuanzishwa kwa kiwanda hicho katika wilaya ya Namtumbo kitaleta faida kubwa sio kwa wilaya ya Namtumbo bali hata mkoa mzima wa Ruvuma kwani kitakuwa na uwezo wa kuajiri zaidi ya watu 150 kwa wakati mmoja.
Alisema, kujengwa kwa kiwanda hicho kitasaidia kupunguza adha wanayokutana nayo wa kulima na wajasirimali wadogo kufuata vifungashio mbali na mkoa wa Ruvuma kwa gharama kubwa, jambo linalochangia sana kurudisha nyuma juhudi za wakulima na wajasiriamali.
Alisema, ujenzi wa kiwanda hicho ni kuunga mkono Utekelezaji wa agizo la Rais wetu Dkt John Pombe Magufuri la Tanzania ya viwanda na kuwataka wakulima kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na kutunza miundombinu ya kiwanda hicho ambacho kitakuwa mkombozi mkubwa kwao.