Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akikabidhi msaada wa chakula kwa watoto yatima kwa Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Shinyanga Society Orphans, Bi. Ayam Ally Said aliyepokea chakula hicho kwa niaba ya baadhi ya vituo hivyo mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha Shinyanga Society Orphans, Bi. Ayam Ally Said alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa msaada wa chakula mbele ya vyombo vya habari Mkoani humo.
Chakula na kukabidhi. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akikabidhi msaada wa chakula kwa watoto yatima kwa Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Shinyanga Society Orphans, Bi. Ayam Ally Said aliyepokea chakula hicho kwa niaba ya baadhi ya vituo hivyo mkoani Shinyanga.
********************************
Na Anthony Ishengoma- Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack ametoa wito kwa wadau kujitokeza kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwani watoto hao walitamani kuwa na wazazi lakini Mungu hakuwapa mapenzi hayo na kutaka anayeguswa ajitokeze kusaidia watoto hao.
Bi. Telack ametoa shukrani zake kwa wasimamizi wa vituo vya kulelea watoto yatima kwa kazi kubwa wanayofanya kulea watoto na moyo wao wa kuhakikisha wanawasaidia waweze kupata maisha na pengine waweze kufikia ndoto zao.
Bi. Telack ametoa msaada wa tani 1.7 za mchele yenye thamani ya shilingi Milioni 3.1 kwa ajili ya vituo vya kulelea watoto yatima mkoani Shinyanga mapema jana katika Ofisini kwake ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata huduma ya chakula.
Makabidhiano kama hayo tayari yalifanyika kwa baadhi ya vituo Mkoani hapa wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona na msaada huu ni mwendelezo wa kutoa misaada kama hiyo kwa makundi yenye mahitaji maalum.
“Katika kipindi tulichotoka cha Corona watu wengi waliokuwa wanasaidia wameondoa misaada yao na sisi kama mkoa tukaona tuangalie namna ya kusaidia ili watoto hawa waendelee kuishi,naomba wadau wajitolee ili kusaidia watoto hawa waweze kuishi na kuendelea kusoma wakiwa na mahitaji ya vifaa vya shule”,alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Bi. Telack aliongeza kuwa Mkoa wa Shinyanga una vituo vingi vya kulelea watoto ikiwemo Shirika lisilo la Kiserikali la Agape ACP ambalo tayari lishapewa msaada wa vyakula wanaojihusisha kulea na kuwapa elimu watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, na kituo cha Shinyanga Society Orphanage Centre kinacholea watoto wasio na wazazi.
Akipokea Chakula hicho kwa niaba ya vituo vitatu vya kulelea watoto yatima, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kituo cha Shinyanga Society Orphans, Bi. Ayam Ally Said alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano anaoendelea kuwapatia kwa kutembelea kituo chake mara kwa mara na kutoa msaada wa vyakula na nguo.
Alisema zaidi ya kupewa msaada wa chakula sasa wanahitaji msaada zana za kufanyia kazi wajitegemee ili watoto wafanye kazi, wawe watoto bora na baadaye kuwa wafanyakazi bora wa serikali.
Wakati huo Bi. Ayam aliongeza kuwa Shinyanga Society Orphanage Centre haihitaji kuwa tegemezi nakudai wanaweza kulea watoto hao vizuri kama serikali inaweza kuwapa zana za kufanyia kazi kwani maeneo ya kuzalisha chakula na mali wanayo bali wanachoitaji ni msaada wa trekta ili waweze kujitegemea.
Vituo vya kulelea watoto yatima vilivyonufaika na msaada huo ni Shinyanga Society Orphanage Centre cha Mjini Shinyanga na Muvuma na Peace Kahama Orphanage Centre vya Mjini Kahama.