Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Bibiana Bundala akikabidhi shilingi milioni 16 kwa uongozi wa Mbulu Vijana SACCOS.
**************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kupitia Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mbulu, Bibiana Bundala amekabidhi shilingi milioni 16, 6 kwa Mwenyekiti wa Mbulu Vijana SACCOS Justine Sulle kwa niaba ya SACCOS hiyo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza Desemba 4 amesema fedha hizo zimerejeshwa na TAKUKURU toka kwa wadaiwa sugu wa SACCOS hiyo ambao walikopeshwa mwaka 2014/2015.
Makungu amesema awali fedha hizo zilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ikiwa ni mikopo kwa vijana kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbulu,
Amesema kwamba walikopeshwa vijana wanachama wa SACCOS hiyo kwa sharti la kurejeshwa fedha hizo baada ya mwaka mmoja ili iweze kupewa makundi mengine yenye uhitaji.
Amesema hata hivyo vijana hao baada ya kupokea mkopo huo waligoma kurejesha hadi TAKUKURU ilipoingilia kati mwezi Novemba 2020 kwa kuwasaka vijana hao na kuwabana kurejesha fedha hizo.
Amesema wamefanikiwa hayo na Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mbulu Bibiana Bundala amezikabidhi kwa Mwenyekiti wa SACCOS hiyo Desemba 4.
“Tunatoa rai kwa kundi la vijana mkoani hapa, pale Serikali inapowakopesha fedha kupitia programu mbalimbali ikiwemo asilimia 10 inayotengwa na halmashauri, wafanyie miradi ya maendeleo kisha warejeshe na kupewa mikopo zaidi ili kukuza biashara zao,” amesema Makungu.
Amesema kundi la vijana limekuwa na changamoto katika kurejesha mikopo inayotolewa na Serikali ukilinganisha na makundi ya wanawake na walemavu.
“Hivyo ni rai yetu kundi hili lijifunze kwa makundi ya hayo namna yanavyofanikiwa katika kurejesha mikopo,” amesema Makungu.