Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Bw. Joseph Haule, akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) ambaye pia ni Mjumbe wa bodi hiyo Arch. Elius Mwakalinga, wakati wajumbe wakikagua hatua za ujenzi wa upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara – Kibaha (km 19.2), jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati wa ziara yao ya kukagua hali ya mtandao wa barabara kwa mkoa huo na kutembelea hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara – Kibaha (km 19.2), jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, akiwaonesha wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (hawapo pichani) jiwe linalotumika katika ujenzi wa upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara – Kibaha (km 19.2), jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa hatua za ujenzi wa upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara – Kibaha (km 19.2), ambao umefikia asilimia 96 na kutarajiwa kukamilika mwezi Machi 2021.
Msimamizi wa Kitengo cha Mizani ya Vigwaza Eng. Charles Ndyetabula, akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati wajumbe hao walipokuwa wakikagua mzani wa Vigwana na kujionea namna ya magari yanavyopimwa katika mizani hiyo iliyopo mkoa wa Pwani.
…………………………………………………………………………………………….
Serikali imesema kuwa uwepo wa teknolojia mpya ya utengenezaji barabara hapa nchini utasaidia kuzuia kubonyea kwa barabara kutokana na kwamba teknolojia hiyo imezingatia viwango vya magari yenye uzito mkubwa na ongezeko ya idadi ya magari.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, mara baada ya kukagua upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha kuwa njia nane yenye urefu wa kilometa 19.2, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Bw. Joseph Haule, amesema kuwa utekelezaji wa teknolojia hii katika miradi ya barabara nchini utasaidia kuokoa fedha za matengenezo ya barabara, hali itakayoruhusu miradi mingine ya barabara kuendelea kutelekezwa nchini.
“Utaalamu wa teknolojia hii uliotengenezwa na Wizara ndio unaotumika katika ujenzi wa barabara hii, nimeagiza kufuatilia na kutunza taarifa za utekelezaji wa mradi huu ili mwishoni tuweze kujua teknolojia hii ina faida kiasi gani na hatimae baadae tutumie katika utekelezaji wa barabara zote nchini.
Aidha, ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kuhakikisha wanatafiti kwa kina kujua namna malighafi zilizopo nchini zinavosaidia katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini badala ya kutumia fedha nyingi kuagiza malighafi nje ya nchi.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ngusa, amesema kuwa upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha kuwa njia nane yenye urefu wa kilometa 19.2 unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani.
“Kama mnavyoona mradi unaendelea vizuri na mkandarasi yupo katika hatua za mwisho kukamilisha mradi huu ambao kwa sasa umefika asilimkia 96”, amesema Mhandisi Ngusa
Katika hatua nyingine wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara walikagua mzani wa Vigwaza, mkoa wa Pwani ambapo waliridhishwa na uendeshaji wa mzani huo kutokana na teknolojia za kisasa za CCTV kamera zilizofungwa hapo ambazo hutoa fursa ya kuweza kufuatilia kazi zinazoendelea kituoni hapo.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wamekamilisha ziara ya ukaguzi wa miradi ya miundombinu katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani ambapo pamoja na mabo mengine wamekagua mradi wa barabara ya Kimara – Kibaha na mzani wa Vigwaza, mkoani Pwani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano