************************************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, leo mchana amekutana na wadau wa sanaa za ufundi na kuahidi kusimamia kivitendo hoja yao ya kutaka Watanzania wengi zaidi watumie kwa wingi sanaa za uchongaji, uchoraji na sanaa nyingine za ubunifu za hapa nchini.
Dkt. Abbasi amejibu kero ya wadau wa sanaa hizo ya kutaka masoko zaidi kwa kuwaahidi kuwapatia wasanii hao eneo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kila kunapotokea michezo waoneshe na kuuza kazi zinazoakisi utamaduni wa Mtanzania.
Aidha, Jioni hii Dr. Abbasi pia ametembelea Tanzania House of Talents (THT) kituo cha ubunifu katika sanaa za muziki kilichoasisiwa na hayati Ruge Mutahaba na kuiahidi familia ya Ruge waliohudhuria akiwemo mama yake mzazi, dada, kaka zake na wasanii wa THT kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha ndoto ya Ruge kusaidia kuinua vipaji vya vijana inaendelezwa.
“Sisi wanadamu ndio tunafika mwisho lakini siku zote ndoto kuu hazifi, niko hapa leo kuwaahidi kuwa mimi na wenzangu wengine wengi nitakaowakusanya wakiwemo wasanii waliopita hapa THT tutashirikiana nanyi kuiendeleza THT,” alisema na kuagiza Wizara yake kukiunganisha Kituo hicho na Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TasuBA) ili kuwa na ushirikiano katika mafunzo kwa vijana wenye vipaji. Aidha, ameahidi kutoa mchango wake katika vifaa vinavyohitajika katika kituo hicho.