………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mradi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Mv. Kilindoni Hapa Kazi Tu kitakachokuwa kinafanya safari kati ya kisiwa cha Mafia na Nyamisati umefikia asilimia 98 na kwamba ifikapo Desemba 15 mwaka huu kitaingia majini kwa mara ya kwanza.
’’Wana-Mafia tumekuwa tukizungumza sana sasa tumefikia hatua kwamba kivuko chetu kimeshakamilika bado asilimia mbili ambazo ni kazi ndogo na haya ni matokeo ya mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana.’’
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2020) mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia-Nyamisati katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Mradi huo unajengwa na kampuni ya M/S Songoro Marine Boat Yard ya Mwanza kwa gharama ya sh. bilioni 5.3.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inatarajia kivuko hicho kitakuwa kimeshaanza kazi wakati wa sikukuu ya Krismas ya mwaka huu. “Tatizo la usafiri kati ya Mafia na Nyamisati litakuwa historia baada ya kivuko hicho kukamilika na kuanza kazi.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kwa kuwapongeza Watanzania kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu jambo ambalo limezaa matunda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle alisema hadi sasa mkandarasi ameshakamilisha kazi zote kubwa ikiwemo ufungaji wa mfumo wa injini, usukani, mabomba ya maji, viti, milango, vyoo na upakaji wa rangi.
Mtendaji huyo alisema kazi zilizobaki ni ufungaji wa vifaa vya kuongozea, ambapo tayari vifaa hivyo vimewasili nchini tangu Desemba 2, 2020 ili kukamilisha ujenzi wa kivuko hicho ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja kuanzia sasa.
Amesema baada ya kazi ya ujenzi wa kivuko hicho kukamilika kitafanyiwa vipimo na wataalamu kutoka Chuo cha Bahari (DMI) pamoja na kufanyiwa uhakiki wa usalama na wataalamu kutoka Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kabla ya kuanza kazi ya kutoa huduma.
Kivuko hicho cha MV Kilindoni kina urefu wa mita 39, upana wa mita 12 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0.70 hadi mita 1.8 na kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100, yaani abiria 200, magari madogo sita. Kukamilika kwa kivuko hicho kutafungua fursa za kibiashara katika kisiwa cha Mafia na kutaondoa adha ya usafiri kati ya Nyamisati na Mafia.