Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa haki za Watu Wenye Ulemavu duniani katika kuadhimisha “Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu” ikiwa na kauli mbiu “Si Kila Ulemavu Unaonekana”.
Chimbuko la siku hii linatokana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 47/3, la 1992 ambalo liliipitisha siku ya Desemba 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya maadhimisho ya Watu Wenye Ulemavu Duniani. Lengo la maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii katika nchi husika kutambua, kuheshimu na kutetea haki na fursa sawa, ushiriki wa Watu Wenye Ulemavu katika masuala ya maendeleo, mahitaji yao, kutafakari changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kukabiliana nazo.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, inaendelea kutetea haki za Watu Wenye Ulemavu na kuweka msukumo wa utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9/2010 na miongozo ya kimataifa na kikanda.
Tume inazipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi mbali mbali zinazozichukuwa katika kuboresha haki na fursa za Watu Wenye Ulemavu nchini.
Pamoja na pongezi hizo kwa Serikali, Tume inatambua juu ya kuwepo Watu Wenye Ulemavu unaoonekana. na usioonekana. Aidha, Tume inatambua kwamba Watu Wenye Ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za kiafya, elimu, ajira, unyanyapaa na unyanyasaji. Kwa muktadha huo, Tume inatoa rai kwa Serikali kuendeleza juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wanawekewa mazingira mazuri ya kupata mahitaji yao kulingana na hali zao za Ulemavu unaowakabili. Aidha, Tume inawataka wananchi wanaoishi na Watu Wenye Ulemavu kuchukua hatua za kuwasaidia na kuwaona kuwa sehemu yao.
Tume inawataka pia Wananchi kuachana na imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya Watu Wenye Ulemavu kuvunjika moyo na kujiona hawakubaliki, hawawezi na hawana mchango wowote kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.
Kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu, Tume inawasihi Wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao ili kuweza kubaini mapungufu waliyonayo katika viungo vya miili yao na kuchukua hatua stahiki. Tume inaiomba Serikali kuwatumia vyema watalaamu wake kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Ulemavu usioonekana ambapo athari zake zinaweza kumuathiri mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.
Mwisho, Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za Watu Wenye Ulemavu zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa hapa nchini.