***********************************************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani ,Muharami Mkenge, amewataka wafanyabiashara katika bandari jimboni hapo, kuwa watulivu na kwamba kero walizompatia ikiwemo kutozwa kodi kubwa huku miezi miwili sasa hawafanyi kazi anakwenda kuzisimamia ili zipate ufumbuzi.
Mkenge alitoa kauli hiyo bandarini hapo, alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hali ya kibiashara sanjali na kusikiliza changamoto zilizopo, ikiwa na lengo kuhakikisha wafanyabiashara hao wanaendelea na shughuli zao huku wakilipa kodi ya Serikali.
“Nimekuja kukutana nanyi ili tuzungumzie hali ya biashara mnazozifanya, zinazosaidia kuipatia mapato serikali yetu, upande wenu mmeniambia changamoto mlizonazo ikiwemo ya kutozwa kodi kubwa na kero nyingine,” alisema Mkenge.
Aliongeza kwa kusema kuwa yeye hana uwezo wa kutoa maamuzi, hivyo atakutana na viongozi husika kuhusiana na hilo, na kwamba yatayokuwa juu ya uwezo wao atakwenda kuzungumza na Mawaziri na Rais Dkt. John Magufuli ili kuhakikisha wanaendelea na shughuli zao.
“Nashuhudia hali ilivyokuwa ngumu hapa bandarini, hakuna pilikapilika za kazi zilizokuwepo hapo awali hii ni dhahiri kabisa kwamba serikali haikusanyi kodi kutokana na kutokuwepi kwa shughuli zinazofanyika,” alisema Mkenge.
Awali wakizungumza kwa niaba ya wenzao, Majogo Majogo, Kingi Mohamed, Mohamed Rashid na Mahona Joseph walieleza, wanatozwa kodi kubwa hivyo kushindwa kuendelea na biashara, na kwamba wana miezi miwili sasa hawana kazi.
“Kama unavyoiona hii ndio hali ilivyo kuna hali mbaya sana Mheshimiwa Mbunge, sisi wenye bodaboda tunaporudi nyumbani tunapofunga mlango kisha tunaweka madumu ya maji ili mlango kujihami na wizi, waliokuwa hapa bandarini wamekwenda kuiba majumbani,” alisema Majogo.
Kwa upande wake Mahona Joseph alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na kusitishwa utaratibu wa awali wa kulipia kodi zao benki, ambapo kwa sasa haupo hivyo wanawasubiri wafanyabiashara wakubwa walete mizigo ndio nao wapatekazi.
Kuhusiana na malalamiko ya ushushaji wa mbao na miti Mkenge aliwataka vijana hao kugomea kiwango hicho, hali itayorejesha kiwango kinacholingana na ugumu wa kazi wanazozifanya.