Mwalimu mkuu wa shule ya awamu na msingi Kazamoyo English Medium (Kwa Mwalimu Samwel) ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Alphaxad Mramba (kushoto) akizungumza jana na wanafunzi wa shule hiyo juu ya kusoma kwa bidii na kuwasikiliza walimu ili waendelee kufaulu na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa iliyoshikwa mwaka huu na wanafunzi wa darasa la saba, kulia ni mhasibu wa shule hiyo Paulo Singo.
Mkurugenzi wa shule ya awamu na msingi Kazamoyo English Medium ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Mwalimu Samwel Mghamba akizungumza na waandishi wa habari baada ya shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2020.
……………………………………………………………………………….
KUSOMA kwa bidii, nidhamu, ushirikiano wa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wadau wa elimu, umechangia shule ya awali na msingi Kazamoyo English Medium (Kwa Mwalimu Samwel) ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kushika nafasi ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu wa 2020.
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi Kazamoyo English Medium, Mwalimu Samwel Mghamba ameyasema hayo wakati akielezea siri ya wanafunzi wa darasa la saba kuongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kufaulu kimkoa na kiwilaya.
Mwalimu Mghamba amesema kwa mwaka huu shule hiyo imeshika nafasi ya 183 kitaifa, nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya kwanza kiwilaya kutokana na juhudi kubwa za walimu, wanafunzi na wazazi, walezi na wadau wa elimu kwa ujumla.
Amesema shule hiyo ina utaratibu wa kuanza kufundisha wanafunzi wa darasa la sita mitaala ya darasa la saba kila mwezi wa 10 pale mtihani wa Taifa unapofanyika na ifikapo mwezi April huwa wameshamaliza.
Amesema kipindi cha likizo ndogo iliyosababishwa na ugonjwa wa covid 19 mwanzoni mwa mwaka huu wanafunzi walifanya mitihani kila mara majumbani kwao na kuwatoa hofu ya mitihani na kuwajengea uwezo zaidi na kujiamini kwenye mtihani wa Taifa hivyo wakafaulu vizuri.
“Shule ya Kazamoyo English Medium ilinunua mashine ya kudurufu karatasi hivyo tukawawekea utaratibu wa wanafunzi kufanya mitihani ya uelewa na juhudi hizo zikaonekana kupitia matunda ya ufaulu mzuri,” amesema mwalimu Mghamba.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Alphaxad Mramba amesema wamepata mafanikio hayo kutokana na walimu wa shule hiyo kufanya kazi yao kwa bidii, umoja na ushirikiano, bila kuchoka, manung’uniko au kutegeana.
Mwalimu Mramba amesema baada ya shule hiyo kuongoza kwa kufaulisha kimkoa na kiwilaya hawatabweteka kwani wataendelea kuwafundisha wanafunzi kwa bidii zaidi.
“Nadhani walimu wa shule nyingine hivi sasa watakuwa wanajipanga kuhakikisha shule zao zinatupiku kwenye nafasi hii nawaahidi wana Mirerani tutaendelea kuwasomesha ipasavyo wanafunzi wetu ili tuendelee kuongoza kimkoa,” amesema mwalimu Mramba.
Mmoja kati ya wanafunzi wa darasa la sita, ambaye atafanya mtihani wa darasa la saba mwakani 2021, Saumu Yusuf, amesema wameshaanza kufundishwa mtaala wa darasa la saba tangu mwezi wa 10 mwaka huu.
Mwanafunzi mwingine wa darasa la sita, Gideon Charles, amesema shule ya Kazamoyo English Medium, maarufu kama kwa Mwalimu Samwel, kwa mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza, kimkoa ikiwemo kufaulisha watoto 12 watakaokwenda kwenye shule za sekondari za vipaji maalum.
Mwanafunzi mwingine wa darasa la sita, Miriam Julius, amesema wanatarajia kufaulu vizuri mwakani kwenye mtihani wa darasa la saba, ili kulinda heshima ya shule hiyo, ambayo kwa mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza, kimkoa na kiwilaya.