Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akielezea jambo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Farkwa katika vijiji vya Bubutole na Mombose kujadili malalamiko yao ya ulipwaji fidia kupisha ujenzi wa bwawa la Farkwa wilayani Chemba.
Mbunge wa Chemba Mhe. Mohamed Monni akiwa na baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Maji wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Nadhifa Kemikimba (hayupo pichani) katika kikao cha kujadili malalamiko ya wananchi wa Farkwa wilayani Chemba
Baadhi ya wananchi wa Bubutole wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika kijiji cha Bubutole wilayani Chemba.
***************************************
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka wananchi wa Farkwa katika vijiji vya Bubutole na Mombose kuwa na subira wakati malalamiko yao yakishughulikiwa.
Mhandisi Kemikimba ameyasema hayo wakati alipokutana na wananchi wa vijiji hivyo kujadili utekelezaji wa mradi wa bwawa la Farkwa na kushughulikia malalamiko ya wastahiki kuhusiana na fidia.
Amesema mpaka sasa jumla ya malalamiko ya wastahiki zaidi ya 400 yamewasilishwa katika ofisi za Mkurugenzi wa Jiji Dodoma na ofisi ya Mkurugenzi imechukua muda mrefu kufanya majumuisho ya majibu ya malalamiko yao kutokana na wananchi kuwasilisha malalamiko kwa awamu na wakati tofauti.
“Natambua moja ya hoja ziliwowasilishwa ilikuwa baadhi yenu hamkuwa mnaonekana kwenye jedwali la fidia la awali na wengine malipo yenu yalikuwa pungufu. Hoja hizi zote zimeshughulikiwa na jedwali la nyongeza la fidia limeandaliwa” Mhandisi Kemikimba alisema.
Kwa ujumla serikali itahakikisha imewalipa wananchi wote waliolipwa pungufu na ambao hawakuwepo katika jedwali la awali la kulipa fidia ili kila mwananchi aweze kupata haki yake inayostahili.
Zoezi la uthamini wa mali za wastahiki lilifanyika na jumla ya bilioni 7.7 zilitengwa kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha eneo la ujenzi wa bwawa la Farkwa na wastahiki 2,769 kati ya 2,868 wamelipwa sawa na asilimia 96.5 ya malipo yote na mpaka sasa fedha zilizobaki ni shilingi milioni 213.7 kwa ajili ya wastahiki 100 ambao bado hawajalipwa.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu ilifanyika kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyoifanya katika vijiji vya Bubutole na Mombose Novemba 21, mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine aliwahakikishia wananchi kwamba hawatahamishwa mpaka miundombinu ya huduma za kijamii katika sehemu wanakohamia kukamilika.