Wahamiaji haramu raia wa Ethiopia wapatao 34 waliokamatwa Desemba 02, 2020 katika kitongoji cha Mwalukonge Kijiji cha Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu wakiwa katika kituo cha Polisi cha Lamadi.
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mwanzalima akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya tukio la kukamatwa kwa wahamiaji haramu raia wa Ethiopia wapatao 34 katika kitongoji cha Mwalukonge Kijiji cha Lamadi wilayani Busega, Desemba 02, 2020 katika . kituo cha Polisi cha Lamadi.
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Maafisa wa jshi la Polisi na Idra ya Uhamiaji wakiwa katika katika Kituo cha Polisi Lamadi Wilayani Busega Desemba 02, 2020 kabla ya Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mwanzalima kutoa taarifa ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu 34 raia wa Ethiopia Desemba 02, 2020 na kupelekwa kituoni hapo.
***********************************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewakamata wahamiaji haramu raia wa Ethiopia wapatao 34 katika kitongoji cha Mwalukonge Kijiji cha Lamadi wilayani Busega.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Desemba 02, 2020 katika Kituo cha Polisi cha Lamadi, Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mwanzalima amesema wahamiaji haramu hao wamekamatwa Desemba 02, 2020 na askari waliokuwa doria .
“ Katika maelezo yao wanasema wametokea Kenya walikuwa wanaelekea Malawi wakisindikizwa na Wakenya wawili, walipofika Lamadi ilitokea purukushani kati yao na wasindikizaji wao baada ya kuwalazimisha kupanda kwenye mitumbwi ili watembee nao ziwani; ndiyo wakakimbia na kuelekea mashambani, bahati nzuri askari wetu walikuwa doria wakafanikiwa kuwakamata” alisema Mwanzalima.
Ameongeza kuwa wahamiaji haramu hao watafikishwa mahakamani kwa kuwepo nchini kinyume cha sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 rejeo la mwaka 2016 kifungu cha 4 hukumu yao ikiwa ni kifungo kisichopungua miaka miwili, huku akibainisha kuwa Vyombo vya usalama vinaendelea kuwatafuta wasindikizaji wa wahamiaji hao na watakapokamatwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Mwanzalima ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu kufanya kazi zitakazowaingizia kipato halali na kuwaonya wasijiingize katika biashara haramu ikiwemo ya kusafirisha wahamiaji haramu jambo ambalo linaweza kupelekea wao kushtakiwa, nyumba na vyombo vya usafiri vitakavyotumika katika biashara hiyo kutaifishwa.
“Natoa onyo kwa Mtanzania yeyote aliyeko Mkoa wa Simiyu atakayejishughulisha kuwasaidia, kuwaonyesha njia ya kwenda popote tukimkamata sheria inasema atafungwa kifungo kisichopungua miaka 20, atakayewahifadhi kwenye nyumba yake atafungwa na nyumba itataifishwa na serikali; ambaye chombo chake kitatumika kuwasafirisha atafungwa miaka 20, atalipa faini isiyopungua milioni 20 na chombo chake kitataifishwa,” alisema Mwanzalima.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amewataka wananchi kuwa makini na kuhakikisha kuwa wageni wanaoingia katika maeneo yao wanawafahamu na ikitokea kuna watu wanaowatilia shaka watoe taarifa kwa viongozi walio katika mamlaka zao za utawala na viongozi hao washirikiane na vyombo vya usalama ili hatua zichukuliwe haraka.
Mmbaga ametoa wito kwa vijana wa Mkoa wa Simiyu kutumia fursa ya amani iliyopo hapa nchini kuendelea kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kufanya kazi zitakazo waingizia kipato halali na katu wasijiingize kwenye biashara haramu, huku akibainisa kuwa mkoa huo hautawafumbia macho wote watakaojihusisha na vitendo vya biashara haramu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP. Richard Abwao ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale watakapowaona watu wasiowatambua katika maeneo yao ili kuendelea kuimarisha ulinzi wao pamoja na mali zao katika maeneo waliyopo.