*****************************************
Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Joseph Mkirikiti amekagua daraja linaloendelea kujengwa katika Mtaa wa Miomboni na kuwataka Wakala wa Bara bara Mjini na Vijijini (TARURA) mkoani hapo kuhakikisha daraja hilo linakuwa imara ili wananchi wapate huduma muhimu.
Mkirikiti amesema kwa kuwa eneo hilo ni Korofi na lipo katika mkondo wa maji linahitaji umakini mkubwa.
Daraja hilo ni kiunganishi kati ya watu wa Babati Mjini na Mtaa wa Miomboni na Korongo mbili na tatu.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TARURA) halmashauri ya mji wa Babati Innocent Mungi ameeleza kuwa Bara bara ya miomboni ina urefu wa Kilomita 3.28 ambapo inaunganisha bara bara inayoelekea Singida na kuishia kijiji cha Nakwa.
Amesema kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwaka 2019 bara bara hiyo ilikatika baadhi ya maeneo ambapo ofisi ya TARURA Mjini Babati ilifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano na kuendelea kupata huduma zote muhimu kwa kuweka Kalavati la chuma ambalo walilitoa kutoka daraja la Mruki.
Amesema kwa sasa wanasubiri bajeti ya mwaka 2020-2022 ili kuweka box kalavati.
Meneja wa Wakala wa Barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoa wa Manyara Mhandisi Slaa, amesema wakati TARURA inaanzishwa mwaka 2017 haikuwa kwenye mtandao wa barabara za ujenzi Babati Mji hivyo haikuwekwa kwenye bajeti iliyopita ya kwa kuwa ni mpya na kwa sasa watakachokifanya ni kupunguza bajeti iliyotengwa kwa ajili ya bara bara zingine na kuhamishia kwenye zingine ambazo hazikupangiwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Babati mjini mkoani Manyara Pauline Gekul yeye akawapongeza Tarura kwa hatua walizochukua kuwarudishia mawasiliano wananchi kwa kuwa walikuwa wanalazimika kutumbukia kwenye mtaro na kuvutana ili kufika upande wa pili.