Pichani kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini, Bw Godfrey Mngereza akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nafasi Art Space Bw Kitururu kwenye Maonesho ya Museum Art Explosion yaliyofanyika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Wasanii wa kikundi cha Zawose Sisters Kutoka Bagamoyo wakionesha umahiri wa kupiga na kucheza ngoma ya kigogo kwenye Maonesho ya Museum Art Explosion “TUKUTANE DAR” yaliyo fanyika kwenye Theatre ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Mwanamuziki Izack Abeneko kutoka jijini Dar es Salaam akionesha umahiri wa kucheza Saxophone kwenye Maonesho ya Museum Art Explosion “TUKUTANE DAR” yaliyo fanyika kwenye Theatre ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Wazazi mbali mbali wakiwa na watoto wao wakifuatilia Maonesho ya Museum Art Explosion “TUKUTANE DAR” yaliyo fanyika kwenye Theatre ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Wageni mbali mbali wa ndani na nje ya nchi wakifurahia Maonesho ya Museum Art Explosion “TUKUTANE DAR” yaliyo fanyika kwenye Theatre ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
**************************************
Na Sixmund J. Begashe
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Bw Godfrey Mngereza, amelipongeza Shirika la Makumbusho ya Taifa, kwa kuendesha program ya Museum Art Explosion (MAE) inayotoa fursa kwa wasanii wa Sanaa za ufundi na Jukwaani kuonesha kazi zao kila Ijumaa ya Mwisho wa Mwezi kwenye kumbi za Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Bw Mngereza ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam kwenye onesho la MAE kwa kushirikiana na Nafasi Art Space lililobeba kaulimbiu ya “TUKUTANE DAR” Mwezi Novemba 2020 lililofanyika kwenye Ukumbi wa King George kwa upande wa Sanaa za Ufundi (Art Exhibition) na Jukwaa la Kisasa kwa Sanaa za Jukwaani.
“Sina budi kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kuunga Mkono juhudu za Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli za kuwainua Wasanii kiuchumi. Program hii ya MAE imetoa fursa nyingi kwa wasanii na sasa inaendelea kutoa kwa kuwapatia nafasi ya kuonesha kazi zao hapa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, sisi kama BASATA tutaendelea kushirikiana nanyi”. Alisema Mngereza
Akiwakaribisha wageni mbali mbali kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw Philip Maligisu amesema Program hii ya MAE ni moja ya utekelezaji wa kazi za kimakumbusho za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kiutamadani kwa watu mbali mbali hasa kwa watoto.
“Kabla ya Maonesho haya ya Jukwaani, tulikuwa na program maalumu kwa watoto wetu, watoto walipata nafasi ya kufundishwa kupiga na kucheza ngoma zetu za asili na muziki wa asili, pia walipata nafasi ya kujifunza namna ya kuwasilisha mawazo yao kupitia michoro mbali mbali, na sasa tutaona ngoma na muziki wa asili kutoka kwa wasanii wetu, huku kote ni kurithisha na kuudumisha urithi wetu wa utamaduni” Aliongeza Bw Maligisu.
Bw. Mgereza na Maligisu kwa pamoja waliupongeza uongozi wa Nafasi Art Space kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa katika kufanikisha Maonesho hayo, pia waliwapongeza sana wadau mbali mbali waliojitokeza kushuhudia maonesho hayo, na kuwashauri kuendelea kuunga mkono kazi za wasanii kwa kuudhuria kwa wingi kwenye maonesho yanayofuata ndani ya Program hiyo ya MAE.
Nao wasanii waliopata fursa hiyo waliushukuru uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuwajali wasanii nchini kwa kuwapa fursa ya kuonesha kazi zao za sanaa kwenye Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni huku wakiahidi kuendelea kufanya kazi za sanaa na utamaduni zinazozingatia maadili na utamaduni wa Mtanzania.
“Tulisikitishwa sana na program hii iliposimama, lakini sasa tunaipongeza Serikali kwa kutujali pia kuujali utamaduni wetu, Makumbusho ndio sehemu sahihi kwetu kuonesha kazi zetu, hata kwenye Makumbusho za wenzetu huko nje wanafanya hivi hivi hasa kuvutia watu wengi kutembelea Makumbusho zao, kwakweli nimefarijika sana”. Alisema Msanii Izack Abeneko.
Katika maonesho ya mwezi wa Novemba, wasanii mbali mbali wa Sanaa za Ufundi kutoka Iringa, Morogoro na Dar es Salaam walishiriki na kwa upande wa Sanaa za Jukwaani walioshiriki ni Abeneko Kutoka Dar es Salaam Ashimba Kutoka Zanzibar, Zawose Sisters Kutoka Bagamoyo, Shine Dance kutoka Dar Es Salaam, Theresa Ng’ambi kutoka Zambia, na onesho lijalo la MAE linatarajiwa kufanyika mwenzi Januari 2021.