Na Dixon Busagaga-Kilimanjaro
BARAZA la Taifa la Watu wanaosihi na Virusi vya Ukimwi
(NACOPHA) limepongeza hatua ya serikali kuendelea kutoa bure Dawa za kufubaza
virusi vya Ukimwi kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo ,dawa zinazotajwa kuongeza
seli za kupambana na maambukizi (CD4) kwa haraka ukilinganisha na dawa
zilizokuwa zikitolewa hapo awali.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu
wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini (NACOPHA) Leticia Mourice wakati wa
kongamano lililoshirikisha viongozi wa dini mbalimbali katika kijiji cha jamii kilichopo
uwanja wa Mandela mjini Moshi ambao maadhimisho ya siku ya Ukiwmi Duniani
yanafanyika kitaifa.
“Nina ishukuru Serikali kwa kuendelea kutupatia dawa bure
ambazo kwa kweli dawa hizo ni nzuri sana ,ni tofauti na zile ambazo tulikuwa
tuna meza siku za nyuma ,zinapandisha CD4 haraka ,zinaboresha afya haraka
,yaani pongezi nyingi sana kwa serikali “ alisema Leticia.
Alisema uwepo wa kijiji cha jamii katika maadhimisho ya siku
ya ukimwi duniani kumechangia wengi wa washiriki kufahamu mambo mengi kuhusu
Ukimwi kutokana na mijadala katika kijiji hicho ambapo pia washiriki walipata
nafasi ya kuuliza maswali .
“Naamini kabisa kila mmoja wetu amevuna chochote ,tumekuwa
na viongozi wa dini kwenye mjadala na
wamewaeleza vijana na watu wazima kwamba miili yetu ni hekalu na hili hekalu
linapaswa kuwa safi na tunapaswa kuitunza miili yetu .”alisema Leticia .
“Sambamba na hilo tumepata maelezo mazuri kabisa kutoka kwa
viongozi wetu wa dini ,sasa kutokana na majadiliano haya mnatakiwa kuwa
mashujaa wa kusema hapana ,sihitaji,sipendi kwa habari ya ngono isiyo salama na
msiende kuwa mashujaa wa kuwa na watu wengi wa kucheza nao shoo.”aliongeza
Leticia.
Mkurugenzi wa Tume ya taifa ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS)
Dkt Leonard Maboko akatumia jukwaa hilo kuwaeleza viongozi wa dini kuwa mlango
uko wazi kwa tume anayoingoza endapo kuna masuala mbalimbali ambayo wanegpenda
kuyafahamu zaidi.
Kongamano hilo ni muendeleze wa mambo kadhaa yanayofanyika
ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa
yanafanyika mjini Moshi katika uwanja wa shule ya msingi Mandela uliopo kata ya
Pasua.
Mwisho