……………………………………………………………………………………..
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amesema atahakikisha anakula sahani moja na watumishi wa Halmashauri hiyo wasiotekeleza ilani ya CCM na kutimiza ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi.
Ole Sendeka ameyasema hayo wakati akiwashukuru wananchi wa Kijiji cha Lerumo kata ya Ruvu Remiti alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo na kuwashukuru kwa kumchagua.
Amesema atashirikiana kikamilifu na watendaji wote wa serikali kwa asilimia 100 wanaoamini na kutii maelekezo ya Rais John Magufuli na ambao wenye nia njema ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM.
Amesema watumishi wasioelekea kwenye kutekeleza ilani na ahadi walizoahidiwa wananchi kutoka siku ya kwanza wajue atawasonga hadi dakika ya mwisho.
“Nataka niwaambieni awamu hii ya tano kipindi cha pili ambacho mimi ni mbunge nitashirikiana na watendaji wote wa serikali kwa asilimia 100 wanaoamini na kutii maelezo ya Rais John Magufuli na ambao wanania njema ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM,” amesema Ole Sendeka.
Amesema watumishi wa serikali ni marafiki zake na kuanzia siku alipoapishwa mpaka siku atakapomaliza kipindi chake ila wale ambao hawataelekea kwenye kutekeleza ilani na kutekeleza ahadi walizoahidi wananchi kutoka siku ya kwanza watambue atawasonga hadi mpaka dakika ya mwisho.
Amesema anaamini madiwani waliopita siyo wala rushwa na wamepata Mwenyekiti wa halmashauri makini Baraka Kanunga na Makamu wake Sendeu Laizer wawajibikaji katika kusukuma vyema gurudumu la maendeleo ya wana Simanjiro.
“Kazi iliyobaki ni madiwani kwenda kushirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri, na nina amini madiwani tulionao siyo wala rushwa hivyo watampa ushirikiano mwenyekiti wa Halmashauri yetu,” amesema Sendeka.
Amewashukuru viongozi wa dini kwa kuwaheshimisha kwa madhehebu yao yote kwa kuwaunga mkono harakati za kuombea kupata uongozi hadi harakati za kushukuru, hivyo wananchi wawaamini viongozi waliopo madarakani kwani watafanya na kutekeleza yote waliyoyaahidi.
Amewashukuru viongozi wastaafu wakiwemo madiwani na wenyeviti wa vijiji kwa kuwaachia alama nzuri wakiongozwa na diwani mstaafu Peter Tendee na kwa wale ambao bado wapo naye madarakani bado wanakibarua chakufanya katika kuwatumikia wananchi.