Mtendaji wa kata ya Mshindo,Bahati Mlaki kulia akimkabidhi hati ya uthibitisho wa kuwa diwani wa kata ya Mshindo Ibrahim Ngwada ambaye amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Iringa.
**********************************
NA DENIS MLOWE, IRINGA
DIWANI wa kata ya Mshindo ambaye pia ni Meya mpya wa Manispaa ya Iringa anayesubiri kuapishwa, Ibrahim Ngwada ametoa wito kwa wananchi kumpa ushirikiano katika kuwaletea maendeleo wakazi wa kata hiyo na manispaa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa cheti cha uthibitisho cha udiwani wake katika ofisi za kata za Mshindo, Ngwada pamoja na kutaka ushirikiano amewaahidi kutekeleza ahadi zote ambazo alizitoa wakati wa kampeni kwa ajili ya wananchi wa kata ya Mshindo.
Alisema kuwa atatoa ushirikiano kwa kila mwananchi na kuwa kiongozi bora ambaye lengo kubwa ni kutatua changamoto zinazokabili manispaa ya Iringa na kuwa mfano bora katika maendeleo nchini.
Alisema kuwa ana deni kubwa kwa wakazi wa kata ya Mshindo na manispaa kwa ujumla kutokana na kumwamini na kumpa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu, upande wa madiwani na uchaguzi wa meya uliofanyika wiki iliyopita hivyo jukumu kubwa lilobaki ni kuanza kazi kwa nguvu zote.
Ngwada ambaye amejitokeza kuwa moja ya madiwani wenye msimamo mkoani Iringa katika suala la maendeleo alisema kuwa ushindi wake katika nafasi ya Umeya ni ishara tosha kwamba wananchi wana Imani naye na chama kwa ujumla.
Alisema kuwa deni hilo atalilipa kwa kufanya kazi kwa nguvu zake zote na akili ili kuleta tija kwa wananchi wa kata ya mshindo na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kutojutia kukichagua chama cha mapinduzi.
Alisema kuwa moja ahadi alizotoa ni kuwaunganisha wanawake kutengeneza vikundi ambavyo vitakopeshwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo wanawake, mikopo ya pikipiki kwa vijana na kuwaanzishia biashara ya kuosha magari kwa baadhi ya vijana walioomba.
Aidha alisema kuwa atahakikisha miradi ya maendeleo inafanyika kwa kasi Zaidi chini ya serikali ya awamu ya tano na kuwashukuru wananchi kwa kuweza kukiamini chama cha Mapinduzi hali ambayo itawafanya wahakikishe uchaguzi ujao wanaibuka kidedea.
Aliongeza kuwa moja ya ahadi zao ni wananchi kuwapa kata,ubunge na rais ambapo kama chama kitakuwa na deni kubwa kwa lengo kuyafanya yale ambayo waliahidi wakati wa kampeni, hivyo miaka mitano mliotupa ni kipima tosha cha kutekeleza yale yote tulioahidi.