Baadhi ya mameneja, wakuu wa vitengo na menejimenti ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jeshi la Zimamoto mjini Dodoma.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA)
………………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuanza mara moja kuagiza vipuri kutoka kwa kampuni mama na kuachana na mazoea ya kuagiza vipuri hivyo kutoka kwa watu wa kati ambao mara kwa mara wamekuwa wakilalamikiwa kutoa vipuri ambavyo sio halisi na hivyo kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu huduma za karakana zinazotolewa na Wakala huo hasa upande wa vipuri.
Akizungumza katika kikao kazi cha Wakala huo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu mjini Dodoma mwishoni mwa wiki hii ambacho kilihusisha menejimenti ya Wakala, Wakuu wa vituo vya Uzalishaji vya TEMESA pamoja na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi, Katibu Mkuu Mwakalinga alisema anataka kuiona TEMESA inaendelea kusonga mbele kwa kuboresha huduma zake na kutoa huduma zilizo bora kwa mustakabali wa taifa.
Katika hatua nyingine, alimuagiza Meneja wa Ununuzi na Mkurugenzi wa matengenezo ya magari kuandaa ripoti itakayoonyesha akiba ya vipuri vilivyonunuliwa kwa kila kituo cha karakana ya TEMESA ikionyesha vipuri gani vimenunuliwa na pia vimenunuliwa kutoka kwa mshitiri gani.
‘’Nitatuma timu yangu ya ukaguzi kuona kama hivyo vipuri ni halisi (genuine) na kama vipuri hivyo sio halisi nitavirudisha na hela atarudisha’’, alisisitiza Arch. Mwakalinga ambapo alimuagiza Meneja wa Ununuzi wa Wakala huo kukamilisha ripoti hiyo ifikapo tarehe 6 mwezi Disemba ambapo timu yake itaanza rasmi zoezi hilo la ukaguzi wa vipuri kwa kila karakana.
Aidha, Arch. Mwakalinga pia aliagiza karakana zote ambazo bado hazijafunga kamera za uchunguzi (CCTV) kuhakikisha zinafunga kamera hizo haraka iwezekanavyo ambapo alimuagiza Mtendaji Mkuu kutoa fedha kwa ajii ya ununuzi na ufungaji wa kamera hizo mara moja ambapo karakana ambazo zitapitiwa na zoezi hilo ni karakana ya Same, Songwe, Ifakara na Kahama.
‘’Nataka mkae kikao kwenye kila karakana na mafundi na muweke wazi kwa mafundi uwepo wa kamera za CCTV ambazo zinaonyesha kila kitu kuanzia gari linavoingia kwa mara ya kwanza, likikaguliwa na mpaka linavyotolewa vipuri hivyo kipuri ukikitoa tunakuona, na ole wako ipatikane umefanya uhuni, unafukuzwa na kufungwa’’. Alisema Katibu Mkuu ambapo aliwataka Mameneja wasiwafiche mafundi ili wajue wanaonekana kwa kila hatua wanapokuwa wanafanya matengenezo ya magari hayo.
Kwa upande wa vivuko, Katibu Mkuu aliipongeza TEMESA kwa kuendelea kufanya vizuri hasa kwenye kutoa huduma hiyo katka maeneo mbalimbali ya nchi lakini akaitaka ianze mara moja kuweka mifumo thabiti ili kupunguza matukio ya upotevu wa mapato.
‘’Nataka muweke mifumo kwenye maeneo ambayo ndio mna ukusanyaji mkubwa wa mapato, Busisi Kigongo, Magogoni Kigamboni na Ukerewe, kule sasa ndio muweke mifumo ili kuziba mianya yote ya kuibiwa mapato ili mpate hela nyingi ya kufidia vivuko vingine ambavyo havifanyi vizuri kimapato’’, alisema Katibu Mkuu ambapo aliagiza mpaka kufikia tarehe 4 Disemba Wakala uwe tayari umeanza kuweka mifumo ya kutumia kadi katika vituo vya vivuko hivyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle, akizungumza katika kikao kazi hicho, amesema Wakala umepanga kuongeza uzalishaji katika matengenezo ya magari kufikia shilingi bilioni 30.24 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ikilinganishwa na shiliongi bilioni 22.24 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo alisema hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 36%.
Maselle amesema kuwa ongezeko hilo wanalolitarajia litatokana na uboreshaji wa huduma za karakana ambao unaendelea hivi sasa katika karakana mbalimbali nchini ikiwemo ukarabati wa majengo na miundombinu ya karakana katika karakana za MT.Depot, Singida, Dodoma, Dar es Salaam (Vingunguti), Mwanza na Mbeya pamoja na ujenzi wa karakana mpya ya Mkoa wa Simiyu inayoendelea kujengwa mjini Bariadi na karakana mpya ya kisasa inayotarajiwa kujengwa mjini Dodoma katika eneo la Kizota.
‘’Tutaendesha mafunzo ya kuwajengea umahiri mafundi wetu kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo hatua ya awali ya utekelezaji wa mpango huo wa asilimia 25% nadharia na asilimia 75% vitendo inaendelea baina ya TEMESA na NIT’’, aliongeza Mtendaji Mkuu ambapo alisema mkakati huo ni kwa ajili ya kuboresha huduma za karakana na kukabiliana na changamoto ya wataalamu na mafundi katika baadhi ya karakana za mikoa.
Aidha Maselle aliongeza kusema kuwa wataingiza kwenye mikataba ya ununuzi wa magari, vipengele vya kuwataka wauzaji wa magari yanayonunuliwa kupitia GPSA, kutoa mafunzo kwa mafundi wa TEMESA pamoja na kutoa miongozo ya ukarabati kwa ajili ya matumizi ya karakana za TEMESA ambapo amesema utekelezaji unaendelea baina ya TEMESA na GPSA.
Mtendaji Mkuu aliishukuru Wizara kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli za Wakala ikiwa ni pamoja na kutoa fedha, ushauri na maelekezo mbalimbali yaliyowezesha kuendelea kuboresha huduma zitolewazo na Wakala.