**********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Klabu ya Namungo imeweza kutamba katika mchezo wake wa awali katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuinyuka Al rabita ya nchini Sudani Kusini kwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Chamanzi Jijini Dar es Salaam.
Namungo ilionesha kandanda safi katika kipindi cha kwanza kwani walifanikiwa kutawala mchezo na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka kupitia kwa mshambuliaji wao Stephen Sey ambaye aliweka kambani mabao yote mawili mnamo dakika ya 20 na 39.
Kipindi cha pili Al rabiti walionesha nao wanahitaji ushindi katika kipindi cha pili kwani walibadilika na kutaka kuutawala mchezo ndipo Namungo ikaamua ifanye madiliko kwa kumuingiza Shiza Kichuya ambaye nae alikuja kuuwasha moto na kufanikiwa kupachika bao dakika ya 64 ya mchezo.
Namungo sasa watahitaji sare ya aina yoyote au kipigo kisichozidi mabao mawili katika mchezo wa marudiano ili isonge mbele.