Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ofisini kwake jijini Dodoma akitangaza ajira zipatazo 13,000 za walimu kwa shule za msingi na Sekondari.Kuona majina,bofya hapa MAJINA YA WALIMU_compressed.pdf
Baadhi ya watumishi wa Elimu kutoka Ofisi hiyo wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga (hayupo pichani) wakati akitangaza ajira zipatazo 13,000 za walimu kwa shule za msingi na Sekondari jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ,ametangaza ajira za walimu wa shule za msingi na Sekondari zipatazo 13,000 huku akiwataka wote walioweza kupata ajira hizo kuripoti ndani ya muda uliopangwa.
Akitangaza mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa walimu hao wanapaswa kuripoti ndani ya siku 14 kuanzia Desemba Mosi hadi 14 na wale ambao watashindwa kuripoti ndani ya muda huo nafasi zao zitachukuliwa na walimu wengine.
Mhandisi Nyamhanga amewataka wote walioteuliwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi ambavyo ni shule za msingi na sekondari na siyo kuripoti katika ofisi za halmashauri huku akitoa onyo kwa wale watakaochukua posho za kujikimu kwa siku saba watakazoenda kuripoti afu wasitokee kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema kuwa maombi yote yalitumwa kwa njia ya mtandao na mchakato wa kuyapata majina ya waliokidhi vigezo ulihusisha wataalamu kutoka TAMISEMI na idara mbalimbali.
Aidha Mhandisi Nyamhanga amesema mgawanyo wa waajiriwa waliokidhi vigezo ni shule za Msingi asilimia 60 ikihusisha madaraja manne (4)na Shule za Sekondari asilimia 40 na madaraja saba(7).
Akitaja madaraja kwa shule za msingi amesema” Walimu daraja la lll A, wenye Astashahada(cheti) ya Ualimu, walimu daraja la lll B wenye Stashahada(diploma) ya Ualimu wa somo la English au aliyesomea Ualimu wa awali,”
“Walimu daraja la lll C, wenye shahada ya ualimu kwa masomo ya English, Civics, General studies, History, Geography na Kiswahili, walimu wa daraja la lll B na lll C waliohitimu Stashahada(diploma) ya Elimu maalumu kwa masomo ya Lugha, Sanaa, Sayansi na Hisabati” amesema.
Ameongeza “Kundi la pili ni shule za Sekondari walimu daraja la lll B wenye Stashahada (diploma)ya Ualimu waliosomea Fizikia, Hisabati, Bailojia, Kemia, Uchumi na Sayansi ya Kilimo.
“Walimu wa daraja la lll C wenye shahada ya Ualimu waliosomea Elimu maalumu kwa masomo ya Kiingereza, Jiografia, Fizikia na Hisabati, walimu wa daraja IIIC wenye Shahada ya ualimu waliosomea masomo ya Fizikia, Hisabati, Kemia, Bailojia.
“Walimu daraja la lll C wenye shahada ya ualimu waliosomea masomo ya Sayansi ya Kilimo, Lugha ya Kiingereza, Lugha Sanifu ya Kiingereza, Kichina, Kifaransa, Utunzaji wa Hesabu, Biashara, Uhasibu na Uchumi.” amesema.
Wengine ni “walimu daraja la lll B waliohitimu Stashahada(Diploma) ya ufundi, walimu wa daraja la lll C waliohitimu shahada ya uhandisi katika fani ya Ujenzi, Umeme na Mitambo, Mafundi sanifu wa Maabara wahitimu wa Stashahada ya ufundi Sanifu Maabara na Stashahada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara” amesema Mhandisi Nyamhanga
Aidha amebainisha kuwa serikali imeweka kipaumbele kuajiri walimu kwa ajili ya shule za Sekondari zenye michepuo ya Sayansi na hisabati, ufundi, kilimo na biashara na maarifa ya nyumbani.
Pia amesema wamezingatia kwa shule zile ambazo hazina walimu kabisa wa masomo husika na kwa shule za msingi wamezingatia Sana shule za vijijini ambazo zinaupungufu mkubwa, na wameajiri kwa kipaumbele cha umri, masomo na kada, utimilifu wa nyaraka.
Wengine ni walimu waliomaliza chuo mwaka 2014 na 2019, waombaji walioomba shule za vijijini shule ambazo hazina ushindani na kwa kufuata kigezo cha ulemavu.
Kuona majina,bofya hapa MAJINA YA WALIMU_compressed.pdf