Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akizungumza na wakulima wa Mbutu wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo katika ngazi ya Mkoa huo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mwaipopo akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha jana Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuzindua msimu wa kilimo kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akipanda mbegu za mahindi katika sherehe ya uzinduzi wa msimu wa kilimo kwa ngazo ya Mkoa jana
Mkuu wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akichimba mashimo ya kupanda mahindi ikiwa ni ishara ya kuzindua msimu wa kilimo kwa Mkoa huo jana
Picha na Tiganya Vincent
…………………………………………………………………………………………….
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA
MKUU wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga wametakiwa kuwasaka na kuwamata wafanyabiashara wasiokuwa na waadilifu ambao wamekuwa wakichukua mbegu za pamba na kuzipeleka katika matumizi ambayo hayakusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo uliyofanyika wilayani Igunga.
Alisema watu hao sio wazalendo na hawataki mema wakulima kwa kuwa wanataka kuhujumu kilimo cha pamba katika Wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
“Wafanyabiashara wa aina hiyo ni wahujumu uchumi na wahujumu maendeleo na sisi kama Mkoa tutaendelea kuwasaka na kuwashughulikia usiku na mchana kwa kuzingatia Sheria” alisema.
Aidha Dkt. Sengati alisema sanjari na hilo aliwataka kuhakikisha kuwa mbolea zinazotolewa zinazouzwa kwa bei elekezi ambayo ni shilingi 57,000/= kwa mfuko wa kilo 50 na sio zaidi ya hapo.
Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa Bodi ya Pamba nchini James Shime alisema kuna baadhi ya watu ambao wakiwarubuni wakulima na kununua mbegu walizopatiwa na Bodi na kuzipeleka katika matumizi mengine kama vile usindikaji wa mafuta.
Alisema watu hao wanafanya hivyo ili kutengeneza upungufu kwa wakulima wakati sio kweli kwani Bodi imeshasambaza tani 10,000 za mbegu kati tani 11,000 zinatakiwa nchi nzima.
Shimbe alisema watu hao ni wahujumu uchumi na baadhi watu wameshakamatwa wakiwa wamepakia mbegu na msako unaendelea.
Naye Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Modest Kaijage alisema ni hatari kutumia mbegu za pamba kwa ajili ya kuzalisha mafuta kwa kuwa zinakuwa zimewekewa dawa ambayo inaweza kuwa na athari kwa watumiaji.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amewaonya wakulima wa pamba ambao hawang’oa masalia ya pamba na kutayarisha mashamba yao kuwa Serikali itawachukulia hatua kwa mujibu Sheria.
Alisema kuendelea kuacha masalia katika shamba ni kutenda kosa na mhusika anaweza kushitakiwa na kuwataka kuyaondoa haraka.