Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiwa na viongozi wengine Mshiriki wa Mafunzo akipokea cheti chake mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo. Baadhi wa washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya Pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.Picha ya Pamoja ya baadhi ya washiriki na wahadhiri kutoka chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto.
*************************************
Na Rosena Suka IJA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare ametoa pongezi kwa Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwa kinara katika kutoa mafunzo ya njia za utatuzi mbadala wa migororo ya ardhi mkoani humo. Pongezi hizo alizitoa alipokuwa anafunga mafunzo Novemba, 27 mwaka huu kwa washiriki thelathini na tatu wakiwemo wanaotoka katika Mabaraza ya Kata, Kijiji na Jumuiya Maridhiano ya usuluhishi wa migogoro ya Ardhi.
Mafunzo haya yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Kilombero katika mji wa Ifakara. Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimepewa jukumu la kuendesha mafunzo na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) likishirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mradi wake unaojulikana kama Msaada wa Kuimarisha Usimamizi wa Miliki kwa Uwajibikaji katika Ardhi, maeneo ya uvuvi na misitu.
Mafunzo haya yamekuwa ni mwendelezo wa mafunzo ya aina hiyo ambayo yalielekezwa kutolewa katika wilaya za mkoa wa Morogoro. Mpaka sasa wilaya za Mvomero, Kilosa na Kilombero zimeshapata mafunzo hayo. Wilaya ya Ulanga pia inatarajiwa kupata mafunzo hayo hivi karibuni.
Akiongea katika hafla hiyo Bwana Sanare alisisitiza kwamba mafunzo haya yasiishie tu kwa wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi. Ameomba mafunzo yaende mbali zaidi, kwa viongozi mbalimbali waliopo mkoani na Halmashauri na ameshauri viongozi wa vijiji pia wapate mafunzo. Katika kusisitiza hilo Mkuu wa mkoa alitoa wito kwa wakuu wa halmashauri zote za Mkoa zitenge bajeti kwa ajili ya mafunzo haya muhimu.
Kwa upande wake Ndugu Justus Mulokozi, Mratibu wa mafunzo amesema ni vema viongozi wa mabaraza ya ardhi katika kata na vijiji hasa upande wa migogoro ya ardhi wanaposuluhisha migogoro wakatafuta chimbuko la migogoro na kuhakikisha katika usuluhishaji madalali hawahusiki na badala yake migogoro hiyo ihusishe wahusika wa suala hilo pekee.