KLABU ya Azam FC imefikia makubaliano ya kuachaana na kocha wake, Aristica Cioaba pamoja na Msaidizi wake mmoja, Kocha wa mazoezi ya viungo, Costel Birsan, wote raia wa Romania.
Taarifa ya Azam FC leo imesema kwamba aliyekuwa Kocha Msaidizi, Mrundi Bahati Vivier ndiye atakayeiongoza timu kuanzia sasa hadi atakapopatikana kocha mwingine Mkuu.
“Tunawashukuru Cioaba na Costel, kwa mchango wao chanya walioutoa kwa kipindi chote walichohudumu ndani ya timu hii na tunapenda kuwatakia kila la kheri popote watakapokwenda,” imesema taarifa ya Azam FC.
Uamuzi huo unakuja siku moja baada ya Azam FC kufungwa 1-0 na Yanga SC, bao pekee la kiungo Deus Kaseke dakika ya 48 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacpouba Sogne katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Cioaba aliyekuwa anaiongoza Azam FC kwa awamu ya pili, tangu arejee ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 50 za mashindano tofauti, akishinda 28, sare 11 na kupoteza 11.