Mkurugenzi mkuu wa The Look Bi. Basilla Mwanukuzi Shayo akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam baada ya kuzindua kambi ya Miss Tanzania 2020 ambayo inaanza leo na kumalizika Disemba 05, 2020. Warembo Miss Tanzania 2020 wakipata picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kambi ya Miss Tanzania ambayo inaanza leo na kufikia tamati Disemba 05, 2020.
***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Waandaji wa Mashindano ya urembo ya Miss Tanzania kampuni ya The Look wamefungua kambi ya Miss Tanzania ambayo inaanza leo Novemba 26 na kufikia tamati Desemba 05 mwaka huu.
Akizungumza na Waandshi wa habari Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi mkuu wa The Look Bi. Basilla Mwanukuzi Shayo amesema mwaka 2020 walifanya mchakato wa washiriki kwa kutumia mfumo wa usaili (Audition) katika kanda 6 za Tanzania ambazo ni kanda ya kati, kanda ya Ziwa,Kanda ya Kaskazini,Kanda ya Mashariki , Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Dar es Salaam.
“Kutoka katika kanda hizo jumla ya washiriki 20 walipatikana na leo hii ndio wameanza kambi maalumu ya mchakato wa kumpata mrembo wa Taifa Miss Tanzania 2020”. Amesema Bi.Basilla.
Aidha Bi.Basilla amesema kila mshiriki alitakiwa kuandaa mradi (Project) iwapo atashinda taji la Miss Tanzania 2020 basi atatumia Mradi huo kuupeleka katika Mashindano ya urembo ya Dunia ambapo Miradi mingi hushindanishwa katika kipengele cha Mrembo na Malengo.
“Washiriki wote hawa 20 wanayo miradi yao na mmoja wao atakaeshinda taji la mremb o wa Taifa Miss Tanzania 2020 atatuwakilisha yeye na project yake hiyo”. Ameeleza Bi.Basilla.