Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Abel Makubi, akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa ASCEND unaolenga katika kuimarisha Tafiti za majaribio ya dawa pamoja na maadili ya tafiti za Afya nchini na kufuatilia usalama wa madhara yatokanayo na matimizi ya dawa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA Bw.Adam Fimbo akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es salaam Picha ya pamoja Mara baada ya uzinduzi huo
Mifumo ya udhibiti wa majaribio ya dawa, vifaa tiba na maadili ya tafiti mbalimbali za afya zinazofanywa kwa binadamu, iliyopo nchini itazidi kuimarishwa zaidi, hatua hiyo inakusudiwa kufanyika na kufikiwa kupitia mradi wa ASCEND.
Kupitia mradi huo, Tanzania imefanikiwa kupata kiasi cha Euro 498750 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 1.27 kutoka EDCTP chini ya European Union (EU), unalenga pia kupunguza muda wa kutathmini maombi ya kufanya tafiti za majaribio ya dawa nchini na hivyo kuwezesha upatikanaji wa vibali vya utafiti ndani ya muda mfupi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Adam Fimbo amesema hayo leo alipozungumza mbele ya Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi wakati wa uzinduzi wa mradi huo ambapo Tanzania imefanikiwa kupata fedha za utekelezaji baada ya kuandika andiko la ombi la mradi.
“Taasisi zinazoshiriki katika mradi huu ni pamoja na TMDA ambayo ina jukumu la kudhibiti kwa mujibu wa sheria, nyingine ni NIMR, Mamlaka ya Chakula na (ZFDA), KCRI, MUHAS, ZAHRI na St. Andrew’s University ya Uingereza,” ametaja Fimbo.
Amesema Tanzania imepata fedha za mradi, kupitia andiko la pamoja na taasisi hizo na kwamba fedha hizo huwa zinatolewa kwa nchi ambazo zimeendelea katika Bara la Europa na katika nchi zinazoendelea ambapo hushirikiana kwa pamoja.
“Lengo la kusaidia kufanya tafiti mbalimbali ili kujenga mifumo na ili iwe thabiti katika kufanya majaribio na tafiti mbalimbali, hivyo, baada ya kuandika andiko la mradi tumefanikiwa kupata fedha kwa utekelezaji wa kipindi cha miaka miwili na nusu kuanzia Novemba hii,” amebainisha.
Ameongeza “Kikubwa tutakachofanya ni kuweza kuboresha mifumo yetu ya udhibiti wa majaribio ya dawa, mifumo ya utafiti namna ya kusoma na kupitisha maombi mbalimbali ya udhibiti wa majaribio ya dawa kabla ya kufanyika nchini.
“Vile vile, kuweka mifumo vizuri ya kufuatilia wale ambao wanaweza kupata madhara wakati wanatumia dawa za majaribio, kimsingi dawa za majaribio unakuwa hufahamu kama ni salama au si salama.
“Kwa hiyo unatakiwa kuweka mfumo ambao utahakikisha wale ambao wanapewa dawa hizo wanabaki kuwa salama bila kupata madhara yoyote, mfumo huo tunao, kupitia mradi huu utatusaidia kuuboresha zaidi ili hatimaye tuweze kulinda wale wote wanaoshiriki tafiti mbalimbali,” amesema.
Amesema kupitia mradi huo, MUHAS utawezesha mafunzo kwa wataalamu mbalimbali waliopo ndani ya mamlaka za udhibiti pamoja na wanaofanya utafiti ili tuwe na uelewa mpana zaidi kwenye masuala hayo.
Fimbo amesema mradi huo unahusisha Tanzania Bara na Visiwani, kwa sababu taasisi zinafanya kazi zinazofanana, ni nchi moja, aidha ni sehemu ya takwa la mradi waliona wakae na kutengeneza mradi huo wa pamoja ili waweze kusaidiana.
“Taasisi zetu zinahitaji kupata msaada zaidi kwa maana ya kuwa na wataalamu wabobezi kwenye kufanya tafiti hizi pamoja na ufuatiliaji wa majaribio ya dawa.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba nchini, kwa mfano Tanzania, TMDA ina jukumu la kudhibiti majaribio ya dawa na tumekuwa tunatoa vibali vya kuruhusu majaribio kuweza kufanyika,” amesema.
Fimbo ameongeza “NIMR pia ni sehemu ya kazi yao wanatoa vibali kuruhusu binadamu kushiriki, kwenye majaribio ya dawa, kwa sababu kuna masuala ya maadili ambayo lazima yafuatwe linapokuja suala la kufanya tafiti kwa watu.
“Mgeni rasmi (CMO) yeye ndiye lazima aidhinishe vibali hivyo kama sehemu ya utaratibu ambao umewekwa ili kuruhusu majaribio kufanyika nchini kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa hasa kulinda wale wanaoshiriki kwenye majaribio haya.
“Hivyo, kuna miongonozo ambayo tutaipitia kuiweka sawa ifanane Zanzibar na bara, na wale wote wanaoshiriki ili hatimaye tuweze kutekeleza yale ambayo tumeyaomba wenyewe na kupata fedha hizi,” amesema.
Akizindua mradi huo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Makubi amezipongeza taasisi hizo kuungana pamoja kuandika mradi huo na kufanikiwa kupata fedha hizo.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imewapa TMDA majukumu mbalimbali likiwamo la kudhibiti viwango vya tafiti mbalimbali hasa hizi zinazolenga kugundua ama dawa au vipimo ambavyo vinaweza kutumika kwa binadamu.
“Ili utafiti ukamilike lazima upitie hatua mbalimbali kabla binadamu wengi kutumia hizo dawa au vipimo, katika hiyo ‘process’ tunaanza na watu wachache ambao huwa wanajitolea.
“Baadae ikionekana haiona madhara ndiyo inaenda hatua za mwishoni kuruhusu kutumika hiyo dawa au vipimo.
“Tunashukuru TMDA na taasisi nyingine za tafiti zimeweza kuunganisha nguvu zao kwa pamoja chini ya project hii, ambayo itaupa uwezo TMDA kufanya jukumu lake la usimamizi na udhibiti vizuri, pia na kuziwezesha taasisi zetu kwa maana ya mafunzo,” amesema.