*****************************
Na Jonas Kamaleki, Dodoma
Uvuvi ni “chimbo jingine la thamani” kama ilivyo Tanzanite, Dhahabu na Almasi kwa kukuza haraka uchumi wa Tanzania endapo utasimamiwa na kudhibitiwa kwa umakini.
Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na bahari, maziwa, mito na mabwawa ambavyo vikitumiwa vizuri kwa shughuli za uvuvi vitainua uchumi wa nchi na kupunguza umaskini wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni akilihutubia Bunge la 12 wakati akilizindua alisema kuhusu sekta ya uvuvi,“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na mabwawa. Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira. Hata hivyo, kwa sasa, mchango wake bado ni mdogo. Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu, ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi.”
Kuhusu kuthamini na kuamini kuwa uvuvi utakuza uchumi wa nchi kwa kasi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameunda Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi. Wizara ambayo Dkt. Mwinyi anaamini itakuwa mkombozi wa uchumi wa nchi hiyo.
Uchumi wa Bluu unajumuisha utalii, uvuvi na mafuta na gesi. Kwa mujibu wa Dkt. Mwinyi bahari haijatumika jinsi inavyopaswa kutumika hasa kwenye uvuvi. Anasema Zanzibar inabidi ijipange kufanya uvuvi wenye tija hasa kwenye bahari kuu, uvuvi huu utachangia kwa kiwango kikubwa kukuza pato la Taifa na hivyo kuboresha maisha ya Wazanzibar.
Ujenzi wa bandari za uvuvi na viwanda vinavyotumia malighafi zipatikanazo baharini wakiwemo samaki vitasaidia kukuza uchumi wa Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mtazamo wa Dkt. Mwinyi unafanana na wa Dkt. Magufuli kuhusu kukuza uchumi kutokana na uvuvi.
Akitilia mkazo juu ya ukuzaji uchumi kwa kutegemea uvuvi, Rais Magufuli anasema, “Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Shughuli za Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2018; shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu zinaweza kuingizia Serikali mapato ya moja kwa moja ya takriban shilingi bilioni 352.1 kwa mwaka endapo mifumo ya usimamizi na udhibiti ingekuwa imara na samaki wangechakatwa hapa nchini. Hata hivyo, mapato yaliyokuwa yamekusanywa kwa kipindi cha miaka tisa (2009 hadi 2017) yalikuwa shilingi bilioni 29.79, sawa na shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka. Kiwango hiki cha mapato hakikubaliki.”
Rais Magufuli anazidi kubainisha kuwa Serikali inataka kwenye miaka mitano ijayo, kuisimamia vizuri shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu ili Taifa linufaike na rasilimali zake, kwa kuhusisha sekta binafsi. Kwa bahati nzuri, tayari, mwaka huu (2020) imetungwa Sheria Mpya ya Kusimamia na Kuendeleza ya Uvuvi wa Bahari Kuu.
“Aidha, tumepanga kununua Meli 8 za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika IFAD (4 upande wa Zanzibar na 4 upande wa Tanzania Bara) ili zishiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu. Kama mnavyofahamu, suala la uvuvi wa bahari kuu ni la Muungano. Tunakusudia pia kujenga Bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa ajira zipatazo 30,000; na tutaendelea kuihamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata samaki”, anaongeza Rais Magufuli.
Sambamba na kusimamia Bahari Kuu, Serikali imejipanga kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) pamoja na Mito mikubwa kama vile Ruvu, Rufiji, Malagarasi, Kagera na Kilombero. Wavuvi wadogo watahamasishwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupatiwa mitaji, ujuzi, vifaa na zana za uvuvi; na halikadhalika. Serikali imejipanga kupitia upya tozo na maeneo mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia uwekezaji. Uhamasishaji wa watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa kutumia vizimba utafanyika.
Sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi. Nchi ndogo ya Norway ambayo haina maziwa wala mito kama Tanzania sekta ya uvuvi ni ya tatu kwa bidhaa za nchi hiyo zinazouzwa nje baada ya mafuta/gesi na metali. Hivyo sekta hiyo inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo. Tanzania haina budi kuwekeza zaidi na kusisimamia “chimbo hilo la uvuvi” kwa ajili ya uchumi endelevu na wenye tija.