Promota Evarist Ernest (Katikakati) akiwatambulisha mabondia Ibrahim Class (kushoto) na Simon Ngoma ambao watapanda ulingoni Ijumaa Novemba 27, 2020 kuwania ubingwa wa dunia wa uzito wa Superfeather wa chama cha GBC kwenye ukumbi wa PTA.
*************************************
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Bondia wa Tanzania, Ibrahim Class amesema atamaliza pambano lake la Ijuamaa Novemba 27, 2020 dhidi ya mpinzani wake Mzambia Simon Ngoma mapema zaidi na kutwaa tena ubingwa wa dunia wa uzito wa super feather wa GBC.
Mabondia hao wanapanda ulingoni jioni hii kwenye ukumbi wa PTA katika pambano la raundi 10 lililoandaliwa na promota Evarist Ernest.
Class alisema kuwa anajua Ngoma ni bondia mzuri, lakini hataweza kutamba kwake na anatarajia kushinda kabla ya raundi ya tano.
“Najua amepania, lakini hataweza kushinda kwani nimejiandaa vilivyo na nahakisha nitashinda mapema zaidi,” alisema Class.
Alisema kuwa mashabiki wake wajiandae kwa sherehe kwani amepania kutoa kipigo kikali kwa Ngoma.
Kwa upande wake, Ngoma amesema kuwa Class ni bondia wa kawaida sana na amekuja kuchukua mkanda huo.
“Najua ameshinda mapambano dhidi ya mabondia wa kawaida kama yeye, mimi ni bondia mwenye uwezo wangu, naomba radhi kwa Watanzania kuwa nitamshikisha adabu Class,” alisema Ngoma.
Promota wa pambano hilo, Evarist Ernest “Mopao” alisema kuwa maandalizi yamekamilika na kuwataka mabondia kuonyesha uwezo wao ili kuwapa burudani safi mashabiki.
Alisema kuwa ameleta mknada mpya ambao mabondia hao wawili wataugombania katika pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na la kusisimua.
Mopao alisema kuwa amewasilisha malipo yote kwa kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBRC) na kazi iliyobaki ni malipo kwa mabondia hao mara baada ya kushuka ulingoni.
“pambano lenyewe ni gumu sana, mbali ya hilo, pia kuna ushindani mkubwa katika mapambano ya utangulizi, hivyo kesho (leo) kutakuwa na burudani ya aina yake,” alisema Mopao.