Akizungumza mkoani hapa jana, Ndahani alisema anaamini kijana yeyote atakayethubutu kujiingiza katika kilimo kamwe hatajutia kutokana na faida kubwa atakayoipata.
“Nawahamasisha vijana wenzangu tujitokeze tukalime, tusiiache mvua hii ikapita bure. Kwa wasio na mashamba wasisite kwenda kukodi…shamba la kukodisha gharama yake ni wastani wa kati ya shilingi elfu 25 na 30 kwa ekari moja,” alisema.
Alisema wakati serikali ikipambana kuhamasisha mageuzi ya kilimo ni jukumu la vijana kuhakikisha wanaunga mkono juhudi hizo kwa kutambua kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.
Ndahani alisema takribani asilimia 60 za malighafi ya viwanda vilivyopo nchini hutegemea kilimo hivyo ni jukumu la vijana kuhakikisha wanakwenda na kasi ya mheshimiwa Rais John Magufuli katika kulifanya taifa hili kuendelea kustawi kiuchumi.
“Niwaombe sana tusiwaachie wazee na wanawake peke yao bali vijana tuingie rasmi shambani tusiache mvua hizi zikapita hivi hivi,”alisema afisa huyo wa vijana.
Alisisitiza mathalani kwa vijana wa mkoa wa singida, wana kila sababu ya kuchangamkia fursa ya kilimo chenye tija kutokana na uwepo wa viwanda vingi vinavyohitaji malighafi, hususan zao la alizeti ambalo ndio zao kuu mkoani humo.
Pia aliwakumbusha vijana kuwa mbali ya alizeti tayari serikali imekwishafungua dirisha lingine kwa kilimo cha korosho kwenye mikoa yote ya Kanda ya Kati ikiwemo Singida, zao ambalo lina usalama zaidi na soko la uhakika ndani na nje ya nchi…na kwamba wasichelewe kuchangamkia fursa hiyo ili kuondokana na umasikini na kuinua kipato.
Ndahani ambaye ameshawahi kushiriki kwenye timu maalumu ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru miaka ya hivi karibuni, alisema anaamini misingi bora ya taifa lolote lenye amani, utulivu na usalama hutokana na watu wake hususan vijana kujikita ipasavyo katika uwajibikaji kwenye nyanja mbalimbali-ikiwemo shughuli za kilimo.