Na Ahmed Mahmoud Arusha
Waandaaji wa Mafunzo ya kamati za maafa wametakiwa kuwawezesha na kusogeza mafunzo kamati za maafa hadi ngazi ya kata kuongeza wigo mpana kwa kuwa wao wapo karibu zaidi na jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro Simon Msoka wakati akifunga mafunzo ya kamati za maafa kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha yaliofanyika jijini Arusha kwa siku tatu.
Alisema kuwa mafunzo kama hayo yakisogezwa kwa ngazi za chini zaidi yatasaidia kuongeza wigo mpana wa kupambana na maafa majanga mbalimbali kwa.kuwa wao ndio wapo sehemu kubwa mitaani karibu na jamii zetu.
“Utoaji wa taarifa unaanzia ngazi za chini halafu zinatufikia sisi hivyo uratibu kama huu unatakiwa uanzia ngazi hizo za.chini utasaidia kukabiliana na kuwa na ushirikiano mpana utakaosaidia kufika kwa haraka katika maeneo yatakayoripotiwa kuwa na majanga”
Kwa upande wake Mratibu wa Upunguzaji Athari za maafa ofisi ya waziri mkuu Ally Mwatima alisema kuwa kamati za maafa za mikoa ziandae mipango ya.kujiandaa na kukabili maafa kabla maafa hayajatokea jambo litakalosaidia kupunguza athari za.majanga ya maafa ikiwemo vifo na upotevu wa mali.
Alisema kuwa kamati hizo za mikoa yote nchi zitumie mafunzo waliopata kuelimisha kamati za maafa ngazi za chini bila kungojea mafunzo kama waliopata kwani ofisi ya waziri mkuu imetoa mafunzo hayo kwao kwa lengo la kuongeza wigo mpana wa kukabiliana na Athari za maafa na majanga katika mikoa yote nchini.
“Ngazi za mikoa tayari zimepata mafunzo ya kukabiliana na maafa,hivyo msisubiri mafunzo kama haya kwenda ngazi za chini mnatakiwa kuchukuwa hatua za haraka kutoa elimu mliopata kufikisha ngazi za chini”