Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Prudence Costantine (katikati) akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu jijini Dar es Salaam Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili kushoto ni Mkurugenzi wa Legal Services Society (LSF) Lulu Ng’wanakilala na kulia ni Mkurugenzi wa Wiladf Anna Kulaya
Mkurugenzi wa Legal Services Society (LSF) Lulu Ng’wanakilala (kushoto) akifafanua masuala mbalimbali ya kisheria wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu jijini Dar es Salaam Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili.Mkurugenzi wa Wiladf Anna Kulaya (katikati) akifafanua masuala mbalimbali ya jinsia Shirika lake linavyoshirikiana na Serikali katika kupambana na kutokomeza vitendo vya Ukatili wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu jijini Dar es Salaam Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili.
**********************************
IMEELEZWA kuwa mfumo wa maisha na tamaduni za jamii nyingi nchini, ndiyo msingi wa kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, huku hofu na aibu ya kuchekwa zikiwa sababu zinazowafanya wanaume kuendelea kufanyiwa vitendo hivyo bila kuripoti katika mamlaka zinazohusika.
Kwa mujibu wa Wataalamu wa Masuala ya jinsia, jamii zinaamini kuwa mwanamke anapaswa kuwa na sifa za upole, unyonge, unyenyekevu na nyinginezo huku mwanaume akitakiwa kuwa jasiri, mwenye mamlaka na mtoa maamuzi, mambo ambayo yanachagiza unyanyasaji wa wanawake.
Akizungumza katika semina maalumu ya Waandishi na Wahariri wa Habari, iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na Save the Children, Mshauri Mwandamizi wa Masuala ya Jinsia na Afya ya Jamii Dk. Katanta Simwanza, alisema sababu zinazochangia kukithiri kwa matukio hayo ni mfumo wa maisha na imani za jamii nyingi nchini.
Alisema Tanzania mwanaume anaaminiwa kuwa mkamilifu wa jinsia yake endapo atakuwa na sifa ya ujasiri, ukali, uongozi, mwenye maamuzi na mwenye mamlaka wakati mwanamke anaaminiwa kuwa mnyenyekevu, mwenye heshima, mpole na msikivu imani ambazo zinaashirikia ukandamizaji.
Dk. Semwanza, aliongeza kuwa kwa namna inavyoaminika nchini, mwanaume ama mwanamke akikosa sifa hizo, hutafsiriwa kutokuwa na haki ya kuwa wa jinsia husika.
Aliongeza kuwa vivyo hivyo ndivyo ilivyo hata katika malezi ya familia, ambapo mwanaume analelewa katika misingi ya ujasiri hali ambayo inawafanya wayaishi maisha hayo hata katika maisha na familia zao.
“Kuna wakati mtoto wa kiume anaadhibiwa nyumbani anazuiliwa kulia kwa sababu yeye mwanaume, hii inawajengea ukimya na roho za ukatili,” alisema.
Alisema kwa sababu hiyo ndiyo maana wanaume wengi hukumbwa na vitendo vya unyanyasaji huku wakishindwa kuweka bayana kwa mamlaka zinazohusika.
Kulingana na Dk. Semwanza, sababu nyingine zinazowafanya wanaume kushindwa kuripoti pindi wanapokumbwa na matukio ya unyanyasaji ni hofu za kuchekwa na jamii.
“Inaaminika kuwa mwanaume ni kila kitu, ikitokea amepigwa na mwenzi wake inakuwa nguvu kueleza kwa sababu atachekwa kwamba inawezekanaje mwanaume anapigwa na mwanamke haya pamoja na mambo m,engine ndiyo yanayochangia kutotolewa kwa tarifa za unyanyasaji wa wanaume,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa WiLDAF Anna Kulaya, alisema kuelekea kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia, shirika hilo limedhamiria kueneza elimu kwa jamii ya kuongeza uelewa juu ya msuala ya ukatili wa kijinsia.
Alisema kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) na itadumu kwa siku 16 hadi Desemba 10, mwaka huu.
Prudence Constantine, ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasilinao Serikalini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema kwa kipindi cha miaka mitano cha muhula wa kwanza wa serikali ya awamu ya tano, mengi yamefanyika kukomesha vitendo hivyo.
Alisema pamoja na mambo mengine serikali imeendesha mpango wa kitaifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, unaolenga kupunguza kasi ya vitendo hivyo kwa asilimia 50 hadi 2025.
Constantine, alisema jambo jingine ni kuanzishwa kwa kamati za ulinzi katika ngazi zote kwa ajili ya kushughulikia masuala ya ukatili wa jinsia kadhalika, kuanzishwa kwa madawati ya jinsia 420.
Alisema madawati hayo yamewezesha wahanga 58,056 kuripoti matukio mbalimbali huku Jeshi la Magereza likianzisha madawati 162 katika mikoa yote nchini.
Aliongeza kuwa, utolewaji wa elimu bila malipo ni miongoni mwa mambo yaliyochagiza uwiano wa utolewaji wa haki hiyo kwa jinsia zote hivyo umesaidia kupunguza ukatili wa kijinsia.
Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni ‘Tupinge ukatili wa kijinsia mabadiliko yanaanza na mimi’.