Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa madaktari na wauguzi tarajali.
Wataalamu tarajali wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo katika Hospitali ya MNH-Mloganzila.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ufundi wa Hospitali ya Mloganzila, Mhandisi . Veilla Matee akiwasilisha mada kuhusu matumizi na utunzaji wa vifaa vya hospitali vikiwemo vifaa tiba.
Mkuu wa Idara ya Uuguzi, Ubora na Mazingira wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Bi. Clauda Miombo akiwasilisha mada kuhusu huduma bora kwa wateja.
………………………………………………………………………
Wataalamu wa afya walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (tarajali) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kujituma na kufanya kazi kwa nidhamu ili kupata ujuzi utakawawezesha kutoa huduma bora kwa jamii.
Wito huo umetolewa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi wakati akifungua mafunzo kwa njia ya vitendo yatakayo fanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja chini ya uangalizi wa wataalamu wabobezi.
Dkt. Magandi amewasisitiza kutumia muda wao kujituma zaidi kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu katika kipindi chote watakapokua kwenye maeneo yao ya kazi.
“Mwaka mmoja ni kipindi kifupi sana hivyo nawasihi mjitume kwa bidii na kufanya kazi kwa nidhamu na maarifa ya hali ya juu na kufuata taratibu na miongozo ya afya” amesema Dkt. Magandi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ufundi wa Hospitali ya Mloganzila, Mhandisi. Veilla Matee amewasisitiza watalaamu hao kutumia vifaa kwa uangalifu na kutoa taarifa pale kifaa kinapopata hitilafu ili kifanyiwe matengenezo.
“Hospitali yetu ina vifaa tiba vya kisasa na gharama ya matengenezo ni kubwa hivyo tunapaswa kuvitunza ili viendelee kufanya kazi kama ilivyokusudiwa pia muhakikishe mnatoa taarifa mapema kifaa kinapopata hitilafu za kiufundi ili tushughulikie kwa wakati ’’amesema Bi. Veilla.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uuguzi, Ubora na Mazingira Bi. Clauda Miombo ameshauri wataalamu tarajali kufanya kazi kwa kujiamini na kutoa huduma bora kwa kuwajali wateja, kuwahudumia kwa usawa bila kujali muonekano, kutambua mahitaji na kuwa na mpangilio mzuri wa kazi.
Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo huduma bora kwa wateja, utunzaji wa vifaa, kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na namna bora ya kuwasiliana mahala pa kazi.