Na Mwandishi wetu, Mirerani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imefungua ofisi yake Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, hivyo kuwarahishia wananchi waliokuwa wanataka huduma yao kusafiri kwenda makao makuu ya Mkoa wa Manyara, Mjini Babati au makao makuu ya wilaya hiyo Mji mdogo wa Orkesumet.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari November 24.
Makungu amesema kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo anawahamisha wananchi kuwa jengo hilo litakuwepo eneo la one step centre ndani ya ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite, mji mdogo wa Mirerani.
Makungu amesema kabla ya kuanzishwa kwa ofisi hiyo wananchi wa eneo hilo waliokuwa wanahitaji huduma za TAKUKURU iliwalazimu kusafiri umbali wa kilomita 122 hadi Orkesumet na kilomita 235 hadi mjini Babati.
Amesema ofisi hiyo mpya pamoja na kushughulikia kero za wananchi wa Mirerani, kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 pia itakuwa na majukumu ya kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kwenye majukumu ya kila siku ya eneo la ukuta wa machimbo ya Tanzanite.
“Kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo tunatoa shukrani kwa Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula na uongozi wa Wizara ya Madini kwa kupata ofisi hii itakayoweza kuwahudumia wananchi na kushiriki ulinzi wa rasilimali za Taifa,” amesema.
Ametoa rai kwa wananchi wa Mirerani na maeneo ya jirani kutoa taarifa kwa maofisa wa Mirerani kwa namba +255754819194 au namba 113 isiyolipiwa na wananchi.