**************************************
Na John Walter-Manyara
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) imewasogezea karibu huduma wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa kufungua ofisi katika eneo la Ukuta wa Machimbo ya madini ya Tanzanite.
Taarifa iliyotolewa kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na Mkuu wa Takukuru mkoani hapo Holle Makungu kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo Brigedia Jenerali John Mbungo, imeeleza kuwa ofisi hiyo imefunguliwa katika jengo lijulikanalo kama One Stop Centre na tayari maofisa wa TAKUKURU watakuwa katika ofisi za kituo hicho maalum kuanzia leo Novemba 24,2020 kuwahudumia wananchi.
Kabla ya kuanzishwa kwa ofisi hiyo, wananchi wa eneo hilo walilazimika kupeleka malalamiko yao makao makuu ya wilaya ya Simanjiro mjini Orkesmenti ambapo ni umbali wa Takribani kilomita 122 au mjini Babati makao makuu ya mkoa ambapo ni zaidi ya kilomita 235 kutoka Mirerani.
Makungu amesema ofisi hiyo mpya pamoja na kushughulikia kero za wananchi katika eneo hilo kwa mujibu sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007, pia itakuwa na majukumu ya kushirikiana na vyombo vingine vya usalama katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwenye eneo hilo la ukuta wa machimbo ya Tanzanite.
Aidha TAKUKURU imetoa shukrani kwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Uslama ya mkoa ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti na uongozi wa wizara ya Madini kwa kuwezesha kupatikana kwa ofisi hiyo itakayowawezesha maafisa wa Takukuru kuwahudumia wananchi wa eneo hilo na kushiriki ulinzi wa rasilimali za Taifa zilizopo eneo hilo.
Amesema wananchi wa Mirerani na maeneo jirani wanaweza kuwasiliana na maafisa wao katika kituo hicho maalum Mirerani kwa namba 0754819194 au simu ya bure 113.