Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na Maandalizi ya kuwapokea wanafunzi shule za awali na darasa la kwanza pamoja na wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza Januari mwaka 2021.
Baadhi ywa waandishi na wadau wa Elimu wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga,wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na Maandalizi ya kuwapokea wanafunzi shule za awali na darasa la kwanza pamoja na wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza Januari mwaka 2021.
…………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imewahimiza wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na viongozi wa Mikoa,Wilaya ,Halmashauri na Shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza Januari mwaka 2021 wanaandikishwa na kuhudhuria shuleni kikamilifu.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu tathimini ya Mitihani ya Matoke ya Darasa la Saba.
Mhandisi Nyamhanga amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa Elimu kukamilisha miundombinu kwa kuweka mazingira mazuri ya kuwapokea wanafunzi hao.
“Nawaomba viongozi wakamilishe miundombinu, samani na kuweka mazingira mazuri kuwapokea wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza bila vikwazo vya aina yeyote ili kutekeleza sera ya utoaji wa Elimu msingi bila malipo,”amesema Mhandisi Nyamhanga
Aidha Mhandisi Nyamhanga amewakumbusha viongozi wa Mikoa na Halmashauri kukamilisha maandalizi yote yanayotakiwa kwa ajili ya uandikishaji wa wanafunzi wa shule za awali na darasa la kwanza watakaoanza kwa muhula wa masomo Januari mwaka 2021.
Hata hivyo amesema kuwa Ofisi ya TAMISEMI imeanza uchunguzi wa udanganyifu uliofanyika katika mitihani wa kumaliza Elimu ya msingi mwaka 2020 ambao umesababisha wanafunzi 1,059 kutoka shule 38 kufutiwa matokeo kutokana na tuhuma hizo.
“TAMISEMI inalaani vikali tabia hii ya kukiuka taratibu za ufanyikaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa, na uchunguzi unaendelea na endapo kuna watumishi wa serikali au sekta binafsi watabainika kuhusika serikali itachukua hatua kali,”amesema
Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa Serikali itachukua hatua kali za kinidhamu na sheria ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia hiyo.