Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (katikati) akiwa na Kaimu Kamanda 822 KJ Kiteule cha Tarime Meja MM Kinana ( kulia) alipokagua shamba la kahawa la kikosi hicho lenye ukubwa wa ekari 52 wilayani Tarime mwishoni mwa wiki.
Katibu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa, askari na vijana wa kujitolea alipokagua shamba la kahawa na mahindi la Kiteule cha 822 KJ Tarime ambapo amesema wizara yake itaingia makubaliano na JKT kuanzisha kitalu cha miche bora ya kahawa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kushoto) akiiamba wimbo wa uzalendo na vijana wa kujitolea wakati alipotembelea kikosi cha jeshi 822 Kiteule cha Tarime kukagua shamba la kahawa na mahindi na kuwasihi vijana hao kuwa wazalendo kwa taifa watakaporejea nyumbani kujiajili kwa kuanzisha mashamba yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama chanzo cha maji yanayopatikana katika kambi ya 822 KJ Kiteule cha Tarime ambapo ameahidi kushirikiana na Wizara ya Maji kuwezesha mfumo wa kusambaza maji kwenye makazi na mashamba. Kwa sasa eneo hilo lina tatizo la maji kutokana na kutokuwepo miundombinu.
………………………………………………………………………………….
Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha inawezesha wakulima wengi nchini kupatiwa miche bora ya kahawa imepanga kuingia makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa ili kutumia ardhi yake kuzalisha mbegu za mazao ili kutosheleza mahitaji ya wakulima..
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kukagua shamba la kahawa lenye ukubwa wa ekari hamsini katika kambi ya 822 JKT Kiteule cha Tarime wilayani Tarime.
“Wizara ya Kilimo ipo tayari kuingia makubaliano na JKT kuzalisha miche bora mingi ya kahawa ili kutosheleza mahitaji ya wakulima wa mkoa wa Mara na jirani kwa kuanzia nitatoa shilingi milioni 19 ili TACRI waanzishe kitalu cha miche hapa kambini” alisema Kusaya.
Aliongeza kusema jitihada za Jeshi la Kujenga Taifa Kiteule cha Tarime zinatekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuona majeshi yetu yanajitegemea kimapato kwa kuanzisha miradi ikiwemo kilimo cha kahawa.
Akiwa kambini hapo Tarime, Kusaya alikagua shamba la kahawa ekari 52 zilizopandwa kati ya lengo la ekari 200 na kupongeza jitihada hizo na kuwataka Taasisi ya Utafiti wa zao la kahawa (TACRI) kuanza maandalizi ya kufungua kitalu cha miche bora ya kahawa shambani hapo ili wajitosheleze kwa miche na kugawa mingine kwa wakulima.
“Tutahakikisha tunawasaidia JKT ili wakimaliza kupanda ekari zote 200 kahawa taasisi zetu za TFRA na zingine zitawezesha upatikanaji mbolea na pembejeo ikiwemo mfumo wa umwagiliaji ili shamba hili litumike kama darasa la wakulima wa Tarime kuja kujifunza kilimo bora cha kahawa” alisisitiza Kusaya.
Katika hatua nyingine Kusaya aliagiza Jeshi la Kujenga Taifa kutumia fursa iliyopatikana nchini Misri kuzalisha mahindi ya njano ambayo yanahitajika kwa kiwango cha tani 25,000 kwa mwezi ifikiapo Julai mwaka 2021 kwani wana uwezo huo na wataalam wapo.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda Kikosi cha 822 KJ Kiteule cha Tarime Meja MM Kinana alimweleza Katibu Mkuu huyo wa Kilimo kuwa tayari katika msimu huu 2020/21 wamefanikiwa kupanda ekari 52 za kahawa na mahindi kati ya lengo la ekari 200.
Aliongeza kusema kiteule cha Tarime kina eneo linalofaa kilimo cha kahawa ekari 430 ambapo mkakati wa Jeshi ni kulima eneo hilo kila mwaka kuongeza ekari 50 na kuwa changamoto iliyopo ni ukosefu wa mfumo wa maji ili kumwagilia kahawa wakati wa kiangazi.
“Kiteule chetu tayari tumepanda miche 52,000 ya kahawa na kuwa lengo letu ni kuzalisha wenyewe miche bora ili tujitosheleze kupanda ekari zote 200 na kugawa ziada kwa wakulima wa jirani hivyo tunaomba wizaraya kilimo ituunge mkono” alisema Meja Kinana.
Alitaja changamoto ya upatikanaji mbolea ya kupandia aina ya DAP hivyo kutatiza jitihada za kilimo kwani inayopatikana inauzwa gharama kubwa licha ya serikali kutoa bei elekezi lakini Tarime haifiki alisisitiza Meja Kinana.
Akijibu changamoto hizo za JKT, Katibu Mkuu Kusaya alisema kwanza watashirikiana na wizara ya Maji ili kuona namna ya kuweka miundombinu ya maji kwenye shamba hilo kwa kutumia chanzo kilichopo na hatimaye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itafika kuona namna ya kuwa na mfumo wa umwagiliji kwa njia ya matone ili kahawa ikue vema.
Pili, ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kwenda Tarime kukutana na uongozi wa wilaya na kikosi cha 822 KJ kujua mahitaji ya mbolea na kuwasaidia kuagiza kwa mfumo ya pamoja (Bulk Procurement Sytem-BPS) ili wapate kwa gharama nafuu na kwa wingi.
Tatu, ameitaka TACRI kuharakisha kufungua kitalu cha miche 250,000 ya kahawa kiteuleni hapo na kuwa ifikapo mwezi Januari 2021 atakwenda tena Tarime kukagua utekelezaji wa maagizo yake.
“Sifa ya jeshi ndio sifa ya nchi hivyo wizara yangu itafanya kila lililo ndani ya uwezo kuzitumia taasisi zake kushirikiana na JKT kukuza sekta ya kilimo na kwamba nitakwenda makao makuu ya JKT kukutana na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Charles Mbuge kujadili mkataba huu wa mashirikiano ikiwemo wa kuzalisha mbegu za mazao mengine ” alisisitiza Kusaya.
Akiwa shambani hapo Kusaya alizungumza na vijana wa kujitolea wanaofanya kazi za shamba na kuwapongeza kwa kuwa wazalendo kulitumikia taifa
Kusaya alisema “nawasihi vijana mkirejea nyumbani baada ya mkataba wenu kuisha nendeni mkawe wazalendo kwa kuanzisha shughuli za kilimo na ujasiliamali kwani miaka mitatu mliyokaa JKT imewafanya muwe wataalam wa kilimo “ .
Aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutoa ajira kwa vijana na kipaumbele ni kwa vijana ambao tayari wameonesha uzalendo na moyo wa kujituma wakiongozwa na waliopo kwenye makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwisho
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
TARIME
22.11.2020